MARUFUKU KUGAWA VIJIJI VILIVYOPIMWA-WILLIAM LUKUVI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvu amepiga marufuku vijiji vilivyopimwa na kupewea hati kugawanywa bila sababu za msingi.

Akizindua uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara na Ngorongoro (Arusha), wakati wa hafla iliyofanyika mjini Mugumu juzi, Lukuvi aliagiza mchakato wa matumizi bora ya ardhi uanzie kwa wananchi badala ya kuanza kwa viongozi.

“Viongozi hasa wa kisiasa tusitumie ushawishi wetu kugawa vijiji kwa lengo la kujijengea himaya kisiasa nyakati za uchaguzi; fedha zinazotumika kugawa na kupima upya vijiji ambavyo tayari vina hati ya usajili zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo,” alisema Lukuvi.

Licha ya ugawaji huo kugharimu fedha za umma bila sababu za msingi, alisema mara nyingi haushirikishi wananchi, pia huibua migogoro ya ardhi hivyo kukwamisha juhudi za Serikali za kumaliza migogoro hiyo.

“Napiga marufuku wataalamu wa ardhi kutumika kulazimisha wananchi kukubali vijiji vyao kugawanywa; hata mipango ya matumizi bora ya ardhi lazima yaanze kuibuliwa, kusimamiwa na kutekelezwa na wananchi wenyewe kwa ushauri wa wataalamu,” aliagiza. Mpango huo wa miaka mitano wa matumiza bora ya ardhi katika wilaya hizo mbili zinazopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti utagharimu Sh63 bilioni zilizotolewa na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Watu wa Ujermani (KFW) na Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS).

Mhifadhi wa Ujirani Mwema kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Nuhu Daniel alisema mpango huo utashirikisha vijiji 40 za wilaya za Ngorongoro na Serengeti.

“Mpango huu ambao tayari umetekelezwa katika vijiji 10 wilayani Serengeti utaondoa migogoro ya ardhi kati ya hifadhi na wananchi, hivyo kuimarisha uhai wa ikolojia,” alisema Daniel.

Meneja Mradi wa FZS, Masigeri Tumbuya alisema taasisi yake imetumia Sh4 bilioni kufanikisha utekelezaji wa mpango utakaoongeza shughuli za uzalishaji katika sekta ya mifugo na kilimo kwa vijiji husika.

Daniel alisema mpango huo utashirikisha vijiji 40 za wilaya za Ngorongoro na Serengeti.

Mbunge wa Serengeti, Marwa Ryoba aliwataka madiwani na wananchi katika eneo la mradi kushirikiana na wataalamu kufanikisha mpango huo utakaomaliza migogoro ya ardhi kuhusu mipaka ya hifadhi na vijiji.

Ofisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Jonas Masingili alisema matumizi bora ya ardhi yatakomesha baadhi ya wajanja kuacha kugawa ardhi za vijiji bila kushirikisha wananchi.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.