KANUNI 7 ZA KUONGEA NA MPENZI WAKO MNAPOKUWA MMETOFAUTIANA



“Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao”-Mtume Paulo, 1 Kor 13:1

“Kumbuka kusema sio tu neno sahii katika mazingira sahii, lakini bado ni vigumu zaidi, kuacha bila kusema jambo baya wakati wa kujaribiwa.” ― Benjamin Franklin


Kwanza

Unapojaribiwa na kukutana na tatizo linalohatarisha uhusiano wenu, mweleze mwenzako. Kunyamazia tatizo kwa hofu ya kumkwaza mpenzi wako ni sawa na kukataa ushirikiano wake katika kulisuruhisha. Kumbuka, kidole kimoja hakivunji chawa. Usiogope. Haitakuwa vigumu kwako kumwambia, kama utajua namna ya kumwambia na sio tu la kumwambia. Lugha ya upendo itamvutia mwenzako akulewe kuliko unapotumia lugha ya malaika au ya“mwenye haki” asiye na upendo. Kwa kuzingatia kanuni zifuatazo za upendo utashangaa maongezi uliyodhani yangekuwa magumu yamekuwa mepesi, huru, na ya kujenga.

1. Anza mazungumzo na mwisho kichwani

Kwanza, hakikisha mazungumzo yako yana lengo mahususi (huwezi kuanza safari na hujui unaenda wapi). Jiulize, mwisho wa maongezi haya nataka haki yangu au amani yetu, nimalizie kuangusha ukuta ulioanza kumegeka au nizibe ufa? Unapojibu ipasavyo, utajiepusha na namna ya kuongea ambayo hayatakufikisha kwenye lengo lako.

Shinda kiu ya kushinda kwa ujuzi wa hoja kama lengo lako ni kurekebisha kasoro; maana, “ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga” (1 Kor 8:1). Nuia kujieleza bila kujionesha mjuaji. Linda hadhi ya mwenzako kwa kutompandia kichwani. Kusudia kumaliza mazungumzo huku kila mmoja wenu anajisikia ameshinda. Usiianzishe mjadala pasipo mwisho huu kama unataka kuboresha mahusiano yenu.

2. Ongea katika mazingira mwafaka

Kama lengo la mazungumzo ni kujenga palipobomoka, utatafuta mazingira ambayo wote wawili yanawafaa kuongea. Utajizuia kuongea wakati unachemka hasira au unaumwa njaa, au una haraka. Kama mwenzako hajisikii kuongea usimlazimishe. Muulize, “mpenzi tunaweza kuongea wakati gani?” Kubalianeni muda ambao mnaweza kuongea mkiwa tulivu na pasipo kuingiliwa. Kama lengo la mazungumzo ni muafaka basi tafuteni mazingira mwafaka.

Tena unaweza kuboresha mazingira ya mazungumzo kwa kuingiza ucheshi. Tania pasipo kukebehi. Si muhimu kuongea na uso mweusi uliokunjana ili kuonesha umeguswa. Mgogoro wenu si mbaya kama unavyofikiri. Kawaida, tatizo ni kubwa kichwani kuliko katika uhalisia wake. Basi, vaa nuru ya uchangamfu hata kama ujisiki nawe utachangamka. Unasema unataka uongee naye ili kutibu ugonjwa ulioingilia uhusiano wenu? Kumbuka: furaha ni dawa. “Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa” (Mithali 17:22)


3. Tawala hisia zako
Pamoja na mazingira mazuri ya maongezi bado hisia kali zinaweza kukurudia unapojieleza. Kweli, una haki kuongea kwa hisia. Ukijinyima haki hiyo unaweza kuathiri afya yako na uhusiano wenu. Lakini pamoja na haki hiyo, unapaswa kuonesha hisia zako kwa kiasi. Unapoangua kilio cha uchungu kila unapoongea; au unapopayuka kelele za kugomba kila unapojieleza, unamtisha mwenzako. Badala ya kutoa hoja ya nguvu hapo unakuwa umetumia nguvu ya hoja kummaliza mwenzako. Endesha maongezi ya maridhiano bila kutumia nguvu ya utisho; maana, “katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu” (1Yoh 4:18)

4. Chagua maneno ya kuongea
Unapotawala hisia zako katika pendo utaweza kuchagua maneno yatakayofikisha ujumbe unaoukusudia. Utafikiri kabla ya kufungua kinywa. Daima jiulize maneno yangu yatasikikaje masikioni mwake. Chagua maneno yatakayopenyeza ujumbe bila kumchoma moyo. Uache ukweli uchome huku ukijizuia ulimi wako kumchoma. Chunga ulimi. Ni kiungo kidogo mwilini mwako lakini ni kama moto mdogo huwashao msitu mkubwa (Yak 3:5)

Ulimi unapoteleza na kudondosha hukumu kwa mtu alivyo badala ya tendo alilofanya ,moto huanzishwa usiozimika upesi. Unaposema, “wewe ni malaya” au “sikupendi” unakuza kichuguu kuwa mlima. Kumbuka neno likiponyoka mdomoni mwako huwezi kulirudisha tena. Haraka haraka katika kuongea haina Baraka. Mpenzi mwenye busara halopoki maneno; isipokuwa,hufikiri kabla hajasema.

5. Pongeza zaidi kuliko kushtumu
Ni rahisi kuyaona makosa ya kulaumu kuliko sifa za kupongeza kwa mwenzako. Lakini, kumbuka hakuna binadamu anayependa kukosolewa—hakuna. Ili umfanye mwenzako awe radhi kukusikiliza unapomkosoa, zoelea kumpongeza kwa mazuri anayoyafanya. Ingefaa usindikize pongezi tano kwa kila jambo moja unalomsahiisha. Mwache akuelewe kuwa wewe ni rafiki wa kumsaidia na si hakimu wa kumtia hatiani.

Hata kama hutajisikia huru au natural kumsifia, jitahidi tu. Jaribu kumsifia mema yake aliyoyafanya (‘nimefurahi ulivyotunza muda”). Mpongeze kwa tabia yake njema (“napenda ulivyo muwazi’) au mwonekano wake (“umenyoa/umesuka nywele vizuri”). Sifa hazitampatia kiburi bali uhakika kuwa unampenda. Wakati huo huo wewe jizuie kujisifia. Hekima ya kale inasema, “mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe”(Mithali 27:2)

6. Kosoa kosa pasipo kumshambulia mkosaji
Unapomhakikishia mwenzako upendo kwa pongezi, wewe na yeye mnakuwa tayari kulikabili kosa linaloharibu uhusiano wenu. Hapo, hakuna anayeshambuliwa isipokuwa kosa lenyewe. Lakini, ni kwa namna gani unaweza kuliongelea tatizo pasipo kuzusha tatizo?

Kwanza, epuka kuanza na kiwakilishi nafsi ya pili, “wewe.” Unapoanza na “Wewe hunipigii simu” unaamsha ndani yake hisia za kuona ameshambuliwa. Si ajabu naye akarudisha mashambulizi, “hata wewe ungeweza kunipigia.” Hoja inayoanza na “wewe” inaanzisha mzunguko wa majibizano usiomaliza malumbano.

Badala ya kuanza na “wewe,” anza na “mimi.” Geuza kidole kutoka kwake na kielekeze kwako; kwa namna hiyo, ukimualika mwenzako atazame tatizo kama ulionavyo wewe. Badala ya kusema “wewe hunipigii simu,” unasema, “[mimi] nimezikosa simu zako, natambua umekuwa na shughuli nyingi.” Tena, tafuta ukimtetea mwenzako kwa huruma unapomuonesha makosa yake naye atavutwa kukuhurumia ulivyoumia. Ushahuri huo ni wa hakika, “kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa” (Mathayo 7:2). Tena, “heri wenye rehema, maana hao watapata rehema”(Math 5:7)

7. Yafikishe mazungumzo katika mwisho wake
Kama mwisho wa maongezi ni rehema, msamaha, na maridhiano, fikisha mazungumzo hapo, umbusu na yaishe. Maongezi yasiyo na mwisho yanachosha kichwa na kufadhaisha roho. Sasa, mnayafikishaje mwisho mazungumzo yenu?

Kwanza, mtaweza kufikia mwisho kama mtabakia katika mada kuu ya mazungumzo. Shindeni jaribu la kuchepukia kwenye mgogoro uliokwisha, bakia njia kuu. Mkiruhusu mazungumzo yaamie kwenye ugomvi mliokwishamaliza, mazungumzo yatawakinai

Tena, mnapomaliza maongezi, yaishe kweli tokea moyoni. Msimezee moyoni ili yaishe tu. Msiondoke kabla ya mazungumzo kuisha. Magugu yanayofukiwa bila kuanikwa juani yatachipuka tu na kusumbua tena.

Niongeze kusema, mtaweza kufika tamati kama kila mmoja wenu yuko tayari kusema, “nimekosa, nisamehe.” Kwa kila mgongano, pande zote mbili zinahusika. Si yeye tu, hata wewe unahusika. Kubali kuwajibika kwa makosa yako kwa kuomba radhi; uwe tayari kumsamehe mwenzako toka moyoni, na mmalize. “Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu”(Mathayo 6:15)

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.