MABALOZI WA USALAMA BARABARANI 'RSA' SHINYANGA WAONGEZA NGUVU KAMPENI YA 'ABIRIA PAZA SAUTI' KUTOKOMEZA AJALI
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Katika juhudi za kuboresha usalama barabarani na kupunguza ajali, Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA) Mkoa wa Shinyanga wameungana na viongozi mbalimbali wa serikali na usalama katika uzinduzi wa Kampeni ya Abiria Paza Sauti, kampeni inayolenga kutoa elimu kuhusu usalama barabarani kwa abiria, madereva na mawakala wa usafiri ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za kupunguza ajali za barabarani.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Mkoa wa Shinyanga, ambapo mabalozi hao walitembelea pia waendesha bodaboda na bajaji katika mkoa huo.
Mabalozi wa Usalama Barabarani, wakiongozwa na Mwenyekiti wa RSA Mkoa wa Shinyanga, Seif Nassor, pamoja na viongozi wa usalama akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, na Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Shinyanga, Denis Magembe, wamesisitiza umuhimu wa usalama wa barabarani.
Mabalozi hao wakiwemo Sebastian Deo, Ramadhani Kaswa, Yudas Karumbete, Chibura Makorongo, Ibrahim Subira, Mfaume Magomba Zahoro, Ichobe Marwa Warioba, na Frank Mshana, wamekemea tabia ya abiria kupandishiwa nauli na kuhimiza matumizi ya tiketi mtandao kama njia ya kudhibiti usumbufu na udanganyifu katika usafiri wa abiria huku wakisisitiza umuhimu wa abiria kufunga mikanda wakiwa safarini ili kujilinda na ajali.
Mwenyekiti wa RSA Mkoa wa Shinyanga, Seif Nassor, amesema kuwa ushirikiano wa jamii yote, kuanzia madereva, abiria, mawakala hadi vyombo vya usalama, ni muhimu katika kupambana na ajali za barabarani.
"Usalama wa barabarani ni jukumu letu sote – madereva, abiria, na watumiaji wa barabara. Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha kuwa barabara zetu ni salama. Abiria wanapaswa kutoa taarifa kuhusu ukiukwaji wa sheria na madereva wanapaswa kuendesha kwa makini ili kupunguza ajali," amesema Nassor.
"Tunaamini kuwa kupitia elimu hii ya usalama barabarani, mafunzo kwa madereva, na uwajibikaji wa abiria, tunaweza kufikia lengo letu la kutokomeza ajali za barabarani",ameongeza.
Latra Yazungumzia Tiketi Mtandao na Udhibiti wa Mwendo wa Mabasi
Kuhusu sheria ya tiketi mtandao, Kaimu Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Shinyanga, Bw. Denis Magembe, amewataka wamiliki wa mabasi na maajenti (mawakala) wao kutekeleza kikamilifu utoaji wa tiketi mtandao kwa abiriakatika kupunguza udanganyifu na kurahisisha usafiri.
"Tiketi mtandao ni muhimu katika kudhibiti bei na kuhakikisha kuwa kila abiria anapata huduma inayostahili. Pia, vidhibiti mwendo vinapaswa kuwa katika hali nzuri na vitumike kila wakati ili kuhakikisha usalama wa safari," amesema Magembe.
"LATRA inaendelea kuhakikisha kuwa bei za usafiri ziko katika usawa na zinahusiana na gharama halisi za uendeshaji wa huduma za usafiri wa barabarani. Hii itasaidia kupunguza malalamiko ya wananchi na kuimarisha usalama barabarani",ameongeza Magembe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, ametoa onyo kali kwa madereva wanaokiuka sheria za barabarani, akisisitiza kuwa uzembe wa madereva unachangia kwa kiasi kikubwa ajali na maafa barabarani.
Amesema madereva wanawajibika kuhakikisha usalama wa abiria na mizigo yao kutoka mwanzo hadi mwisho wa safari.
"Madereva wanapaswa kutambua kwamba maisha ya abiria na mizigo yao yako mikononi mwao, na ni jukumu lao kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria zote za usalama barabarani," amesema Kamanda Magomi.
Ameongeza kuwa abiria pia wanapaswa kuchukua hatua kwa kutoa taarifa pale wanapoona ukiukwaji wa sheria na madereva wanaendesha kwa mwendo hatarishi.
Kamanda Magomi amesisitiza kuwa ushirikiano wa abiria, madereva, na vyombo vya usalama ni muhimu katika kupambana na ajali na kutokomeza maafa yanayotokana na ajali za barabarani.
"Abiria wanapaswa kupaza sauti pale wanapoona ukiukwaji wa sheria. Hii ni harakati ya pamoja ya kuhakikisha usalama barabarani," amesema.
Kamanda Magomi pia amewashukuru wadau mbalimbali, wakiwemo abiria, madereva, na wananchi, kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha kwamba barabara za Mkoa wa Shinyanga zinakuwa salama kwa matumizi ya wote.
Madereva Watoa Lawama kwa Madereva wa Magari ya Serikali
Baadhi ya madereva wa mabasi ya masafa marefu wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuanzisha kampeni hii ya usalama barabarani, huku wakilalamikia baadhi ya madereva wa magari ya serikali ambao wameshindwa kufuata sheria za usalama barabarani.
Madereva hao wamesema kuwa tabia ya madereva hao inasababisha usumbufu na mara nyingine husababisha ajali.
"Madereva wa magari ya serikali wanapozembea, wanatufanya sote tusikiwe na madhara. Sheria za usalama barabarani lazima zifuatwe na kila mtu," amesema mmoja wa madereva wa basi la masafa marefu.
Kwa upande mwingine, Kikosi cha Zimamoto kimebaini kuwa idadi kubwa ya mabasi hayana vifaa vya kuzimia moto, na baadhi ya magari yaliyokuwa na vifaa hivyo, vimekuwa vikionyesha kasoro.
Kampeni ya Abiria Paza Sauti inalenga kutokomeza ajali za barabarani zinazohusisha uzembe wa madereva, ulevi, na kutotii sheria za barabarani. Hali ya usalama barabarani imeendelea kuwa changamoto kubwa katika maeneo mengi ya Tanzania, na hatua hii inakuja ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha hali ya usalama na kupunguza maafa yanayotokea kutokana na ajali.
No comments: