SPIKA WA BUNGE AWAKAANGA MAWAZIRI WA MAGUFULI
Spika wa Bunge, Job Ndugai amewaonya mawaziri kuacha kupiga stori
wanapokuwa bungeni, badala yake wawe makini kusikiliza mijadala na
maswali kutoka kwa wabunge.
Ndugai alitoa onyo hilo jana katika kipindi cha maswali na majibu baada
ya kuwataja baadhi ya manaibu ili wajibu maswali lakini walishindwa
kusimama kwa kuonyesha hawakusikiliza kilichokuwa kimeulizwa na wabunge.
“Waheshimiwa mawaziri acheni kupiga stori ndani ya Bunge, ndiyo maana
mnashindwa kusikiliza kinachoendelea humu, hebu punguzeni na mjikite
katika kusikiliza,” alisema Ndugai.
Kiongozi huyo alianza na naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa
Aweso ambaye alimtaka ajibu swali la nyongeza la Mwantumu Dau Haji (viti
maalum - CCM) ambalo lililenga katika suala zima la upatikanaji wa maji
kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Kabla ya swali hilo, tayari mbunge huyo alishauliza swali la msingi
ambalo lilielekezwa ofisi ya Makamu wa Rais na lilijibiwa na naibu
waziri wa wizara hiyo, Kangi Lugola likihusu masuala la mabadiliko ya
tabia nchi.
Aweso alisimama asijue nini cha kujibu huku akiendelea kutazamana na
Spika Ndugai kwa sekunde kadhaa ndipo akaamuliwa kuketi kwa kuwa alikuwa
hajui swali gani liliulizwa.
“Tatizo lenu mawaziri hamsikilizi kinachoendelea ndani ya Bunge, mnapiga
stori tu. Haya naibu waziri Ofisi ya Makamu wa Rais okoa jahazi hilo,”
alisema Ndugai.
Baada ya maswali kadhaa kupita aliwataka naibu mawaziri ofisi ya Rais
(Tamisemi), Joseph Kakunda na Joseph Kandege kujibu swali la nyongeza
kuhusu umaliziaji wa majengo ambayo yanaanzishwa na wananchi.
“Haya naibu mawaziri Tamisemi, Josephat Kandege naomba ujibu swali hilo.
Kama hujajipanga naomba mwenzako Joseph Kakunda ajibu, jamani ndiyo
haya niliyosema wapo hapa tu lakini wanapiga stori na hawasikilizi
kinachoendelea,” alisema spika.
Ndugai aliwaonya pia wabunge kutozungumza na waziri mkuu na kumtaka
kiongozi huyo wa shughuli za Serikali kuzungusha macho ili kuona namna
ambavyo wabunge walikuwa wamesimama na kutaka kuuliza maswali kuhusu
maji.
“Mheshimiwa waziri mkuu, naomba hao wanaozungumza na wewe wakuache
kwanza, hebu geuka nyuma na uangalie pande zote uone namna ambavyo
wabunge wamesimama kutaka kuuliza maswali kuhusu maji majimboni kwao,
Serikali iangalie jambo hili,” alisema.
Wakati huo spika aliitaka Serikali kutafakari namna ambavyo imekuwa
ikitoa maagizo na amri kila wakati kupitia mabaraza ya madiwani akisema
siyo afya na haijengi.
Alikuwa akitolea majibu mwongozo ulioulizwa na mbunge wa Babati Mjini
(Chadema), Pauline Gekul kuhusu mpango wa Serikali kuagiza wananchi
kuendelea kumalizia majengo ya zahanati, maabara na madarasa
waliyoyaanzisha.
“Ndugu zangu Serikali, anachokisema mbunge ni sahihi maana sasa imekuwa
ni kero kubwa, hebu angalieni jambo hilo kwani kila mahali ni maagizo
maagizo na hata tukienda kwenye baraza la madiwani utasikia kuna ajenda
ya kudumu ambayo ni maagizo, hii inakera jamani,” alisisiza Ndugai.
Pia, aliwataka viongozi kuangalia namna bora ya kufanya ili kufikisha
ujumbe kuliko kuagiza kila mara ambako kunaondoa imani ya wananchi kwa
Serikali yao.
Hata hivyo, alisema kumekuwapo na tabia ya baadhi ya viongozi kujiona
kama miungu watu na wanaamini kuagiza kila wakati kwa kutumia amri ndiyo
itakuwa maendeleo wakati si kweli.
Imeandikwa na Habel Chidawali, Mwananchi
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: