CCM YAMTANGAZA KITILA MKUMBO KUWA MWANACHAMA WAO
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemtangaza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na
Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo amejiunga na chama hicho.
Uamuzi huo wa Profesa Mkumbo kujiunga na CCM ameufanya ikiwa ni siku 39
zimepita tangu alipotangaza kujivua uanachama wa ACT- Wazalendo Oktoba
9.
Taarifa ya CCM aliyoitoa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Singida,
Martha Mlata imesema chama hicho Mkoa wa Singida wanamkaribisha kwa
mikono miwili ili waendelee kuimarisha chama katika mkoa huo.
“Nina furaha kuwatangazia wanachama na wapenzi wa CCM Mkoa wa Singida na
Tanzania kwa ujuma kuwa…Profesa Kitila Mkumbo amejiunga tena na chama
chetu,” amesema Mlata na kuongeza:
“Ni fursa kubwa kwa mkoa kumpokea mwalimu baada ya kumpoteza mwanafunzi siku chache zilizopita.”
Akifafanua zaidi katika mazungumzo na Mwananchi baada ya kutoa taarifa
hiyo, Mlata amesema “Profesa Mkumbo amejiunga wiki moja iliyopita na
amelipita ada yote aliyokuwa akidaiwa katika kipindi chote na na mimi
nilichokifanya ni kuwajulisha tu wanachama wetu kuwa mwana mpotevu
karudi nyumbani.”
Alipoulizwa kama ni njia ya kwenda kugombea ubunge wa Singida Kaskazini
amesema “hapana, pale kuna vijana wengi sana ambao wako tayari
kuwatumikia wananchi, kwanza hawezi kuacha madaraka makubwa aliyopewa na
mheshimiwa Rais, yeye ameamua tu kurudi nyumbani.”
Kuhusu kujiunga CCM huku akiwa mtumishi wa umma, Mlata ambaye ni mbunge
wa viti maalum wa chama hicho amesema hilo halina tatizo kwani hata
alipokuwa ‘uhamishoni’ bado alijipambanua ni mwanachama wa chama fulani
kwa hiyo kurejea nyumbani si kosa.
Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: