TUNDU LISU ASEMA "SERIKALI INA HOFU NA MIMI TLS"


Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Tundu Lissu, amesema ameanza kuogopwa na viongozi wa serikali  baada ya jina lake kuwa miongoni mwa majina matano bora ya wagombea wa nafasi ya urais katika Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kutokana na misimamo yake ya kuitetea Katiba ya Tanzania.

Akizumgumza na waandishi wa habari  Mwanza jana, Lissu alisema  tangu atangaze nia yake ya kugombea urais wa TLS ameanza kuogopwa  kutokana  na kujulikana kwa   misimamo yake kuhusu  masuala ya   sheria,  siasa na  katiba ya nchi hii.

Alisema TLS ina majukumu makubwa katika nchi ya kulinda utawala wa sheria na wanasheria ndiyo wanaojua kuliko mtu yeyote  zinapotungwa sheria mbovu na zile za kikandamizaji, pia wao ndiyo wanapaswa kuwa wa kwanza kuanza kuzipigia kelele sheria hizo.

“Kwa miaka mingi  TLS imeongozwa  na watu ambao hawafikiri kwamba wajibu wao wa kwanza kulinda utawala wa sheria,  wao wanafikiri wajibu wao wa kwanza ni kuwapendeza  wanasiasa na matokeo yake TLS imepotea, wanachoogopa  ni kwamba hii raha ambayo wameipata miaka yote hii wakati  wanasheria wa  TLS wakiwa  usingizini akija huyu Lissu itaisha,” alisema Lissu.

Alisema aligombea nafasi hiyo  baada ya kumsikia Rais Dk. John Magufuli akizungumza mbele  ya watanzania kwamba wakili  yeyote  atakayewatetea  watuhumiwa wanaokutwa na  dawa ya kulevya au nyara za serikali wakamatwe na kuwekwa ndani.

Alisema aliposikia kauli hiyo alicheka na kusema sasa ni wakati wa yeye kuwa rais wa TLS ili kauli za aina hiyo zikome na siku mbili kabla ya Rais Dk. John Magufuli kutoa kauli hiyo,  Bunge lilipitisha sheria ya msaada wa sheria.

“Sheria hiyo inasema mtu yeyote anayefunguliwa kesi ya jinai, au madai kama ni maskini hana uwezo wa kumlipa wakili atapatiwa huduma hiyo na wakili atalipwa  na  mtendaji mkuu wa mahakama.

“Sheria hiyo inampatia haki  mwananchi yeyote atakayekuwa  na kesi ya mauaji, pembe za ndovu au dawa za kulevya  kupata wakili atakayelipwa na serikali.

“Siku mbili baadaye Rais anakinzana na sheria hiyo nilishangaa kweli.  Tayari sheria hiyo imetungwa  ni jambo muhimu kweli kwa sababu katika  nchi hii watu wanasingiziwa sana, kwenye maegereza nyingi   nchini wamejazana wananchi ambao hawana hatia na wapo huko kwa sababu hawakuwa na mawakili wa kuwatetea,” alisema Lissu.

Lissu alisema  endapo atachaguliwa kuwa rais wa TLS atahakikisha sheria ya msaada wa  sheria  inatekelezwa.

Kuhusu hoja ya  Waziri wa katiba na  Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ya kutishia kukifuta chama hicho hicho kwa kuwa kimeanza kujiingiza katika masuala ya siasa, Lissu alisema wanaoleta hoja za kutaka kukifuta chama hicho kama ni wanasheria ujuzi wao wa sheria ni wa shaka lakini kama ni wasiojua sheria wanasamehewa.

Alisema  sheria ya iliyoanzisha TLS inasema mwanachama yeyote aliyekidhi vigezo  vya chama hicho ana haki ya kuwa mgombea wa nafasi yoyote ya uongozi na haijasema  ukiwa mwanachama wa chama chochote cha siasa unapungukiwa sifa  ya kugombea.

“Watu wanazungumza   kana kwamba ni makosa mwanasheria kuwa mwanasiasa, katika nchi hii katiba imeruhusu  siasa za vyama vingi, kuwa wanachamaau  kiongozi wa chama.

“Kuwa tu mwanachama una kuwa na fursa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi serikalini lakini sasa watu wanataka kuaminishwa kuwa ukiwa mwanasiasa huna haki,” alisema

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.