TAKUKURU YAWATAJA WATUMISHI VINARA KWA RUSHWA
WATUMISHI wa halmashauri nchini, wametajwa kuwa ni vinara kwa kuomba aina mbalimbali za rushwa ili kutoa huduma na nafasi za kazi kwa wenye mahitaji.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Handeni, Esta Mulima, wakati wa semina ya maadili ya viongozi wa umma kwa madiwani, wakuu wa idara na vitengo wa wilaya hiyo mjini hapa mwishoni mwa wiki.
Mulima alisema katika halmashauri, baadhi ya watumishi wamejiwekea utaratibu wa kutotoa huduma mpaka wapewe chochote kitu, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za utumishi wa umma.
Alitaja aina za rushwa ambazo wamepata kesi zake kuwa ni rushwa ya ngono hasa kwa watumishi wa kike wanaotaka kwenda kusoma, uhamisho au kupanda vyeo, wakuu wa idara husika huomba rushwa ya ngono kwao ili kufanikisha jambo husika.
Pili wale wanaoomba kazi na zabuni katika halmashauri ni kundi la pili ambalo limekuwa likikumbwa kwa kuombwa rushwa ya kutakiwa kutoa chochote ili kupatiwa nafasi hizo iwe kwa wakuu wa idara au wakurugenzi.
Getrude Cyriacus, Naibu Katibu Sekretarieti ya Maadili Kanda ya Mashariki aliyekuwa akiongoza semina hiyo, alisema:
"Ukiacha vitendo vya rushwa, kitu walichobaini watumishi wengi wamekuwa siyo watunzaji siri za serikali, hivyo kuwataka kubadilika mara moja."
Alisema wapo watumishi mambo yanayojadiliwa kwenye vikao na baadaye huyatoa nje kwa watu wasiohusika kitu ambacho ni kosa kwa taratibu za utumishi wa umma kutoa siri za serikali kwa watu wasiohusika.
Aidha, pia aliwataka madiwani kuacha tabia ya majukumu ya kitaalamu yanapotokea kwani kufanya hivyo kunasababisha baadhi ya watumishi kushindwa kuwajibika vizuri kazini.
Awali, akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, alisema hategemei tena kusikia kuna watu wanaingiliana kwenye majukumu.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi