SABABU ZILIZOMFANYA KOCHA WA MAN U KUTIMULIWA HIZI HAPA

Ole Gunnar Solskjaer alichukua mikoba ya kuinoa Manchester United mwezi Disemba mwaka 2018
Mambo yanaenda kasi sana, na kasi hiyo kwa Manchester United ni ya kushangaza.

Muda mfupi tu uliopita, mambo yalikuwa tofauti sana, kulikuwa na mbwembwe nyingi na shangwe wakati United ilipofanikisha kumrejesha Cristiano Ronaldo mnamo Agosti 27 aliyekuwa anasakwa sana na Manchester City.

Wakati supastaa huyo wa Ureno alipoanza maisha kwa mara ya pili United kwa kufunga mabao mawili katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Newcastle, mambo yote yalionekana kama yako sawa.

Wakati mamia ya mashabiki walisubiri kwa zaidi ya nusu saa kumshangilia nyota huyo wa Ureno alipokuwa akifanya mahojiano baada ya mechi hiyo, ilionekana kuwa jambo lisilowezekana kuwa wiki 10 baadaye, Ole Gunnar Solskjaer angetimuliwa.

Lakini, baada ya kunusurika kutimuliwa kwenye kipigo cha 'fedheha' cha 5-0 kutoka kwa Liverpool mnamo Oktoba 24 na kipigo kingine cha 2-0 kutoka kwa Manchester City mnamo Novemba 6, Solskjaer aliondolewa kwenye kiti cha meneja kufuatia kipigo kingine cha 'aibu' cha 4-1 Jumamosi hii dhidi ya Watford.

Chini yake msimu huu takwimu ni mbaya. Manchester imeshinda michezo minne katika mechi 13 kwenye mashindano yote tangu ushindi huo dhidi ya Newcastle. Wamepata alama 7 kutoka kwa mechi 8 za Ligi Kuu ya Uingereza, huku hawakuruhu bao katika mchezo mmoja tu. Wameruhusu kufungwa mabao kumi na tisa katika michezo saba. Wametolewa katika Kombe la Carabao.

Upande wa pili wa Solskjaer
Kwa wengine, kuondoka kwa Solskjaer walikutarajia muda mrefu. Hawakuwahi kushawishika kuwa Mnorway huyo alistahili nafasi hiyo na wamekuwa wakisubiri mambo yamshinde tangu alipopewa mkataba wa kudumu mnamo Machi 2019.

Hukumu hiyo ni kali.
Solskjaer alirejesha ile munkari ya klabu iliyokuwepo wakati wa siku za mwisho mwisho za enzi ya Jose Mourinho. Bila shaka, alifanya maamuzi kwa manufaa ya Manchester United, klabu anayoipenda kutoka moyoni.

Alifanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Uingereza msimu uliopita, ambayo ni ya juu kwa United tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu mwaka 2013. Baada ya mechi 19, walikuwa kileleni, nafasi ambayo ni adimu na hawakuwa kuifurahia tangu Ferguson aondoke.

Kama wangeifunga Villarreal katika fainali ya Ligi ya Europa kama ilivyotarajiwa, Solskjaer pengine angekuwa na kitu cha kuringia na kujilinda dhidi ya matatizo ambayo yamemkumba.

Lakini De Gea alikosa mkwaju wa penalti huko Gdansk na kama wengine walivyohisi wakati huo, vipigo vingekuwa mwiba kwa Mnorway huyo.

Solskjaer: Yanayotazamwa kama mabaya yake
Solskjaer ameiongoza United kushika nafasi ya pili na ya tatu katika ligi kuu kwenye misimu miwili

Imekuwa dhahiri na kwa muda mrefu kuona ni wachezaji gani anaowaamini na ambao hawaamini. Ni dhahiri, Donny van de Beek anaangukia katika kundi la mwisho la asiowaamini.

Haijabainika kabisa ni jukumu gani Solskjaer alifanya katika kuwasili kwa Van de Beek kwa pauni milioni 35 kutoka Ajax mnamo Septemba 2020, lakini hakuwahi kutoa hisia zozote alizofikiri Mholanzi huyo anaweza kuwepo Old Trafford.

BBC Sport imeambiwa na zaidi ya chanzo kimoja kwamba Solskjaer hakuwa na uhakika kwamba Van de Beek atafanya vizuri uwanjani kutokana na uwoga.

Mtazamo huo ni wa kushangaza kidogo ikizingatiwa karibu kila mechi msimu uliopita ilichezwa kwenye viwanja tupu. Van de Beek kuiingia na kufunga wakati United wakijidhatiti kutafuta njia ya kurejea kwenye mchezo dhidi ya Watford kulidhoofisha mtazamo wa Solskjaer zaidi.

Van de Beek alikuwa miongoni mwa wachezaji kadhaa wa United ambao wamekuwa wakiwekwa benchi msimu huu.

Matumaini ya Dean Henderson kuwania nafasi ya golikipa yamekatizwa, ingawa, inakubalika, David de Gea amekuwa mmoja wa wachezaji waliofanya vizuri zaidi United.

Janga la kutojiamini
Harry Maguire, aliyejiunga Manchester United mwaka 2019 kwa ada ya £80m, alilimwa kadi nyekundu dhidi ya Watford Jumamosi

Mnamo tarehe 12 Novemba, Harry Maguire aliziba masikio kwa vidole vyake - ishara inayofasiriwa kama dharau kwa wakosoaji wake - baada ya kufunga katika ushindi wa 5-0 wa England dhidi ya Albania.

Siku nane baadaye, nahodha huyo wa United alitolewa nje kwa kadi nyekundu akiichezea klabu yake katika kipigo cha Watford.

Mechi hizo mbili zilifunika kiwango cha hivi majuzi cha beki huyo. Mzuri kwa England, mbaya kwa United.

Hilo linaweza kuonekana wakati wa kichapo cha United cha 4-2 katika klabu yake ya zamani ya Leicester mwezi Oktoba, wakati makosa yake yalipowapa Leicester njia ya kurejea kwenye mchezo waliokuwa wakipoteza.

Inaweza kuonekana pia wakati wa mechi ya debi ya Manchester mwanzoni mwa Novemba, wakati yeye na Luke Shaw walipoteleza, na kumruhusu Bernardo Silva wa City kuchukua udhibiti na kufunga.

Maguire na Shaw walionekana kuzubaa, wakingoja mpira utoke nje ya mchezo. Mtazamo huo ulitofautiana sana na Bernardo, ambaye alikuwa na bidii katika kujaribu kufanya jambo fulani litokee.

Aaron Wan-Bissaka hajafanya kubwa la maana msimu huu, na kushindwa kwa Bruno Fernandes kutumia nafasi ya wazi kusawazisha dhidi ya Watford kulikuja baada ya mchezo dhidi ya City ambao alicheza vibaya, kwani mara kwa mara alipoteza mipira.

Haijawahi kuwa wazi kabisa kwa nini United walitumia £47m kumnunua kiungo wa kati wa Brazil Fred, kutokana na kuonekana ni mchezaji wa kawaida sana.

Je, Solskjaer alikuwa tayari kuwapa changamoto wamiliki?
Mojawapo ya shutuma zinazotolewa mara kwa mara kuhusu Solskjaer ni kwamba hana mtindo dhabiti wa uchezaji unaomtambulisha, kumaanisha kwamba yeye ni kocha mwepesi kucheza nae ikilinganishwa na makocha wengine vigogo kama vile Pep Guardiola, Jurgen Klopp na Thomas Tuchel.

Htaa hivyo mtazamo huu unapuuza ukweli kwamba amezifunga timu zinazosimamiwa na makocha hao wote watatu, huku pia akiwafunga Julian Nagelsmann, Marcelo Bielsa na Mauricio Pochettino.

Hapo awali, Solskjaer alihisi kikosi chake hakina utimamu wa kucheza kwa kasi,presha na kushtukiza jinsi alivyotaka. Aliwaondoa kikosini Romelu Lukaku na Alexis Sanchez kwa lengo la kuwa na washambuliaji vijana ambao wanaweza kukimbia na kuwalazimisha walinzi wa upinzani kufanya makosa.

Safu yake ya kiungo bado ilionekana dhaifu, lakini kulikuwa na muundo thabiti wa kusajili kwa Solskjaer. Alimsajili Jadon Sancho mapema mwishoni mwa msimu na kumshawishi Edinson Cavani kusalia Old Trafford kwa mwaka mmoja zaidi wakati ilionekana kuwa raia huyo wa Uruguay alikuwa na nia ya kuondoka

Kuwasili kwa Ronaldo kulibadili mambo.
Cristiano Ronaldo amereja Old Trafford na kuonyesha uwezo wake

Kwa mshtuko, jukumu nambari tisa, ambalo Cavani na Mason Greenwood walitarajiwa kulibeba, lilikabidhiwa kwa mzee huyo wa miaka 36.

Kutokana na hilo, Cavani amekuwa akicheza kwa nadra huku Greenwood akicheza pembeni zaidi,hali inayomkosesha uhakika wa kucheza Sancho.

Uwezo wa Ronaldo hauna shaka na mabao yake yameiokoa United zaidi ya mara moja msimu huu. Lakini kuwapa presha mabeki ili kufanya makosa sio aina yake ya uchezaji kwa miaka 10 iliyopita na hakuna kilichobadilika.

Je, Solskjaer alithamini sana kurudi kwa Ronaldo Old Trafford kama vile watendaji wakuu ambao walijua matokeo ya kibiashara ambayo nyota huyo wa Ureno angekuwa nayo?

Na kama sivyo, alikuwa tayari kusema hivyo?
Hata wakati Solskjaer alikuwa bado katika kazi yake na matokeo yalikuwa yakienda vizuri, vyanzo vichache vilivyozama katika historia ya United, vilijiuliza kama yuko tayari kuingia vita vya ndani kwa kile anachoamini kuwa ni sawa, ikiwa yuko tayari kutoa changamoto kwa familia ya Glazer, makamu mwenyekiti mtendaji Ed Woodward.

Kinadharia, Solskjaer alikuwa mwenye bahati ya kupata kazi hiyo kubwa ya kuionoa United kutokana na uzowefu na wasifu wake wa mdogo kwenye ukocha, na asili yake ilimaanisha kuwa angekuwa mt wa kusema 'ndiyo' kwa kila jambo hata kama haliko sawa kwake.

Pengine inaakisi kwa nini Solskjaer alinusurika kutimuliwa alipochapwa na Liverpool na Manchester City. Inaweza ikawa sababu ya kwa nini United ilimruhusu Antonio Conte kujiunga na Tottenham badala ya kumnunua Muitaliano huyo ambaye ni mtu anayesukuma mambo na kuamini anachoamini.

United sasa wameingia kwenye msako wa kutafuta kocha wa tano tangu Ferguson aondoke.

Na baada ya kile kilichopita kwa makocha wote hao watano, hakuna imani kwamba wakati huu, watampata mtu sahihi.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.