YANGA YASHTUKIA MICHEZO MCHAFU, YAJA NA MBINU MPYA
YANGA imerudi kambini ikiendelea na maandalizi yenye akili kubwa kwa ajili ya mechi ijayo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC, huku kocha Nasreddine Nabi akishikilia msimamo kuwa sio kwamba vijana wake wanakata upepo, ila kuna shida sehemu na ameshaigundua kwa sasa.
Nabi ameiongoza Yanga katika mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu msimu huu kutoka na ushindi ikivuna pointi tisa, lakini kuna kelele nyingi kwamba chama lake linakata pumzi kipindi cha pili na kama wakikutana na timu kali watapasuka vibaya.
Hata hivyo, Nabi alisema jana, haoni kama kikosi kinakata upepo, ila alichobaini wachezaji wake wanaridhika mapema na sasa amewachenjia na kutaka watoe dozi nene kama wanavyofanya Bayern Munich nchini Ujerumani.
Nabi alisema amewaambia wachezaji anataka kuona hawapunguzi kasi baada ya kupata mabao akiitolea mfano Bayern inavyofanya kwa kutopunguza kasi hata kama ikipata mabao ya kutosha - iwe katika Bundesliga au Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Hii dhana tu kuwa timu inakata upepo naona wengi sana wanakuja kwangu na mtazamo wa namna hiyo. Kama makocha ambao tunakaa na hii timu na kuiandaa hilo si sahihi, lakini ipo shida kwa wachezaji wenyewe wakipata bao moja au mawili wanaridhika, jambo ambalo si sawa,” alisema Nabi.
“Ukiangalia mechi iliyopita tulipata mabao haraka, lakini baada ya hapo vijana wakapunguza kasi ya kusaka ushindi zaidi, hii sio mara ya kwanza kufanya hivi.
“Tunahitaji kucheza kwa ubora uleule hata kama tuna uhakika wa ushindi. Unapopunguza kasi ni lazima mpinzani wako unampa nafasi ya kupambana. Nimewaambia wachezaji tunahitaji kuwa na ari kama ya Bayern Munich hata wakipata mabao matano, lakini bado watahitaji mengine.”
AKILI YA SVEN
Nabi amesisitiza tayari ameshapata kikosi cha kwanza, lakini katika hilo hataki kuwaacha wakapotea wachezaji wake ambao wamekuwa hawaanzi kikosini.
Kushtukia hilo, Nabi ameanzisha utaratibu kila baada ya mechi wanayocheza siku ya pili yake watakuwa na mechi ya kirafiki ambayo itakuwa maalumu kwa wachezaji ambao hawajacheza mechi iliyopita.
“Tumeona tuwe na hizo mechi za kirafiki angalau moja au ikiwezekana mbili kila baada ya mchezo wa ligi. Mechi hii itakuwa maalumu kwa wale ambao hawakucheza mechi ya ligi au wakacheza kwa dakika chache.
“Tunatakiwa kuwa na timu bora yenye kila mchezaji aliye tayari wakati wowote, lakini kama tutakuwa tunawapa muda wa kucheza wale wanaoanza kisha tukawasahau hawa wengine iko siku itatupa shida,” alisema.
Staili hiyo ndani ya Yanga akiitambulisha Nabi, lakini hapa nchini ilikuwa ikitumiwa pia na aliyekuwa Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: