BAADA YA SIMBA KUFUNGWA NA WABOTSWANA, MORISON AIBUA JAMBO JIPYA
LICHA ya Simba kuchezea kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, jasho la winga wake Bernard Morrison halikwenda bure mbele ya wataalamu wa soka.
Morrison alicheza kwa kiwango cha juu katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam na ndiye aliyetoa pasi ya bao, lililofungwa na Rally Bwalya, jambo ambalo limempa heshima mbele ya wadau.
Staa wa zamani wa Yanga, Tito Andrew alisema kuwa Simba ilijiondoa kwa uzembe kwenye michuano hiyo, kwani haikuwa na haja ya kutumia nguvu mwanzo mwisho, badala yake ilipaswa kulinda ushindi, ila aliona kuna kitu kikubwa alichokifanya Morrison.
“Morrison ameonyesha ukomavu na maana halisi ya mchezaji wa kigeni, aliujua mchezo unahitaji nini na timu yake inahitaji kitu gani, alivaa roho ya uzalendo kwa timu yake, jambo ambalo lilipaswa kuigwa na wachezaji wenzake kuiga upambanaji wake,” alisema na kuongeza;
“Jambo lililonishangaza kuona benchi la ufundi kumtoa mchezaji ambaye alikuwa anapambana kwa kiasi kile na kuwaingiza ambao wamewapa mwanya wapinzani wao kuwafunga, unapokuwa na mtu kama Morrison akikabwa na wachezaji zaidi ya wawili unawapa mwanya wengine kutumia nafasi ya uhuru kuliona lango,”alisema.
Hoja yake iliungwa mkono na mchezaji wa zamani wa Simba, Shaban Kisiga aliyesema Morrison alifanya majukumu yake kwa asilimia 100 na kwamba kupoteza mchezo kwa timu hiyo hakuwezi kuondoa ubora wake.ADVERTISEMENT
“Jamaa anaujua mpira, anacheza kwa starehe na anaufanya ni rahisi, licha ya kwamba Simba ilipoteza mechi, mchango wake ulikuwa wazi na aliwajibika kwa kujiamini.”
Mchezaji wa zamani wa JKT Queens na Twiga Stars, Asha Rashid ‘Mwalala’ alisema kuwa; “Raha ya soka wanaipata zaidi wale ambao wanatutazama jukwaani, ila kwa Morrison anajipa mwenyewe starehe akiwa ndani ya uwanja, licha ya mchezo kuwa mgumu aliurahisisha, ndio maana baada ya kufanyiwa mabadiliko pengo lake lilionekana.”
Kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Azam FC, Deogratius Munishi ‘Dida’ alisema; “Morrison anatumia akili kubwa ya mpira, anamfanya mchezaji wa upinzani afanye makosa, katika mchezo huo aliwajibika kwa kiwango cha juu na kutoa pasi ya bao alilofunga Bwalya, hivyo kufungwa hakuwezi kufuta ubora wake.”
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: