Leo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Usharika
wa Ebeneezer kumefanyika ibada njema iliyoambatana na matukio mbali mbali
ikiwemo ubarikio wa wanafunzi wa kipaimara,ubatizo wa watoto na watu
wazima,kupokea muumini mpya kutoka dhehebu jingine na sakramenti takatifu.
Akihubiri katika ibada hiyo mchungaji na mkuu wa shule ya
sekondari ya Mwadui YOHANA NZELU, amesema
“Na itakuwa hata siku
za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana, utawekwa imara juu ya vilima na mataifa
yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, njooni
twende juu yam lima kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha
njia zake nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka
sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu kwa mataifa
mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na
mikuki yao iwe miundu, taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala
hawatajifunza vita tena kamwe.” ISAYA
2:2-4
Akaendelea kusema “Kuna vitu vilivyomsukuma Isaya kuandika
haya hasa alipoangalia mazingira ya jamii inayomzunguka. Ndipo akagundua kuwa
watu wamejaa ubinafsi, rushwa,udhalimu na haki imepotea. Watu waliendelea na
desturi za ibada zao, pasipo kuweka uchaji wa ibada. Ndipo Isaya anaanza
kukemea udhalimu, dhuluma, rushwa akitetea maisha ya wanyonge. Anawakumbusha
watu wanaowakandamiza wengine kuwa kuna siku inakuja mwana wa Adamu atakapokuja,
kutakuwa na kusanyiko kubwa ambapo mkuu wa haki atonekana akitenda haki kwa
wote.Kanisa la leo linapitia zaidi ya haya yaliyoonekana katika kipindi cha
Isaya, pengine sasa jamii imeharibika zaidi ya ile ya awali. Kwa sasa watu
hatuishi kwa uchaji wa ibada badala yake tunathamini desturi za dini zetu. Mtu
anataka aonekane akiwa na bahasha walakini uchaji wa ibada ndani yake umepotea.
Hofu ya Mungu imepotea,watu hawamwogopi Mungu. Juzi yametokea maafa Kagera,
pande nne za nchi na hata nje ya nchi watu wakishirikiana na serikali wakaamua
kuchangia ili kuokoa maisha ya watu, kuwapa msaada wa kurudisha miundo mbinu
iliyoharibiwa na tetemeko. Lakini kwa kuwa hofu ya Mungu imepotea, watu wengine
wanaamua kufungua akaunti feki ili kijinufaisha kupitia janga hilo, hii ni
hatari sana kwa maisha yetu. Serikali
inatangaza kuwa wamama wajawazito, watoto na wazee watibiwe bure katika hosptali
za serikali lakini kwa uroho na tamaa ya mali mtu anaamua kujinufaisha kupitia
nafasi hiyo. Unaenda kununua kilo 50 ya
cementi dukani,lakini ukifika nyumbani unakuta kilo ziko 48.
Huu ni udhalimu uliokithiri, hofu imepotea, watu hawamwogopi
Mungu. Bwana anakuja katika utukufu wake kuhukumu katika haki, na kila mtu
atatoa hesabu ya matendo yake. Na katika ujio huo wale ambao wamejiandaa na
kujaa maisha ya toba wao watastahimili na Mungu hataona haya kuitwa Mungu wao,
Mungu atusaidie tuishi maisha ya toba.
Hongereni vijana wa kipaimara kwa kufikia hatua hii, sasa
mnaenda kukutana na jamii kama hii aliyoiandikia Isaya, nawasihi mwende
mkafanikiwe kuwa nuru, chumvi, mkamtumikie Mungu kwa uaminifu. Najua wengine
mtakuwa walimu,wengine viongozi, wengine wafanyabiashara, Jitahidini kwenda
kutenda haki. Wewe utakayekuwa daktari katende haki,watu wakapate faraja
kupitia ninyi. Mkaishi maisha ya toba nay a kumwangalia Mungu daima. Pengine
mtakutana na shida, dhiki na mahangaiko, Mungu akawe msaada wenu mkimtegemea
yeye siku zote za maisha yenu.
MUNGU ALIBARIKI NENO
LAKE AMEEN!!
Msaidizi wa Askofu na Dean wa kanisa kuu Shinyanga akiendesha ibada ya Ubarikio wa wanafunzi wa kipaimara
Mkristo mpya akipokelewa kuwa mlutheri kutoka dhehebu la FPCT
ZIFUATAZO NI PICHA ZA MATUKIO YA UBATIZO
Ubatizo ukiendelea
ZIFUATAZO NI PICHA ZA MATUKIO YA UBARIKIO WA KIPAIMARA