MKUU WA WILAYA MATATANI KWA KUMNADI MGOMBEA UBUNGE

Kitendo cha Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu kupanda jukwaani kumnadi mgombea wa CCM katika Jimbo la Siha, Dk Godwin Mollel kimechafua hali ya hewa baada ya kupingwa na vyama vya siasa huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikisema hakufanya jambo sahihi.

Kitendo cha Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu kupanda jukwaani kumnadi mgombea wa CCM katika Jimbo la Siha, Dk Godwin Mollel kimechafua hali ya hewa baada ya kupingwa na vyama vya siasa huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikisema hakufanya jambo sahihi.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima ameliambia Mwananchi jana kuwa ili Buswelu aweze kuchukuliwa hatua, wenye jukumu la kumshtaki ni vyama vinavyopinga jambo alilolifanya.


Alisema vyama hivyo vinatakiwa kumshtaki katika kamati ya maadili inayoundwa na wajumbe wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi katika jimbo husika na kwamba jambo hilo linapaswa kufanyika ndani ya saa 72, tangu apande jukwaani.


Wakati DC huyo akiibua kizazaa hicho, CCM imeendelea kumnadi Dk Mollel huku katika Jimbo la Kinondoni, wagombea ubunge wa CCM, Chadema na Sau wakiwekewa pingamizi.


Uchaguzi wa Siha na Kinondoni utafanyika Februari 17 na unavishirikisha vyama 12, huku ukitajwa kuwa ni mpambano mkali baina ya CCM na Chadema inayoungwa mkono na vyama vitano vya Ukawa ambavyo ni NLD, NCCR-Mageuzi, CUF upande wa Maalim Seif Sharif Hamad na Chaumma iliyojiunga hivi karibuni.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya waliokuwa wabunge; Mollel (Siha- Chadema) na Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF) kujivua uanachama wa vyama hivyo kwa maelezo kuwa wanamuunga mkono Rais John Magufuli na baadaye kujiunga CCM.

Chama hicho tawala kimewapitisha wawili hao kutetea majimbo hayo, huku Chadema ikimsimamisha naibu katibu mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu (Kinondoni) na Elvis Mosi (Siha).

Buswelu ‘alivyochafua hewa’

Juzi katika uzinduzi wa kampeni za Dk Mollel katika viwanja vya KKKT Karansi Jimbo la Siha, Buswelu alisema Serikali haijaribiwi hivyo ni vyema kila mmoja akahakikisha anadumisha amani na kufanya siasa za kistaarabu katika kipindi chote cha kampeni.

Alisema Dk Mollel ameleta heshima kwa wananchi wa Siha huku akiwataka wananchi wote kumuunga mkono na kuhakikisha anapata ushindi wa kishindo.

NEC ilivyomruka Buswelu

Akizungumza na Mwananchi, Kailima alikiri kitendo alichokifanya mkuu huyo wa wilaya kuwa hakikubaliki na kwamba ni kinyume cha kanuni za maadili, lakini haiwezi kumchukulia hatua.

“Wakuu wa mikoa na wilaya hawaruhusiwi kwenda katika kampeni na akifanya hivyo anakuwa amekiuka maadili ya uchaguzi,” alisema na kuongeza,

“Na kama amekiuka vyama vinavyoshiriki uchaguzi vinapaswa kuwasilisha malalamiko katika Kamati ya Maadili ndani ya saa 72.”

Alisisitiza, “Jambo hili tume hatuingii popote na vyama hivyo vya siasa vinalijua hili. Wanatakiwa kumpeleka kamati ya maadili ambayo wajumbe wake wanatoka katika vyama vinavyoshiriki uchaguzi, lakini iwe ndani ya saa 72 tangu kitendo hicho kilipotokea na wao watachukua hatua.”

Alivitaka vyama vya siasa kutokimbilia kulalamika bila kuchukua hatua kwani kama kuna uvunjifu wa maadili, kamati ina mamlaka ya kuwasilisha hilo katika ngazi nyingine ya kisheria kama polisi au kwa DPP (mkurugenzi wa mashtaka).

Kailima alibainisha kuwa NEC katika barua zao hawakuwazuia wakuu wa wilaya na mikoa kushiriki kampeni, bali waliwakumbusha kutojihusisha na kampeni kwani ni kinyume cha kanuni za maadili.

Vyama vyacharuka

Mkurugenzi wa itikadi, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema, “Kama kweli NEC inasema iliwaandikia barua basi ituonyeshe hizo barua, lakini ichukue hatua kwa mkuu huyo wa wilaya ambaye amekiuka agizo hilo walilolitoa.”

Alisema waliposusia kushiriki uchaguzi wa Januari 13, moja ya sababu ni watendaji wa Serikali kuingilia chaguzi na endapo NEC haitachukua hatua wataeleza watakachokifanya kukomesha tabia hiyo.

“Sheria ya utumishi wa umma inazuia watumishi wa umma kujihusisha na siasa, huyu DC kavunja hiyo sheria na kama kuna usawa katika hili basi mamlaka zimchukulie hatua, anatumia nyenzo za Serikali katika mambo ya siasa, NEC ichukue hatua,” alisisitiza.

Mkurugenzi wa Habari wa CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba, Abdul Kambaya alisema tatizo la wakuu wa mikoa na wilaya ni kubwa.

Alisema viongozi hao wamekuwa wakichangia uchaguzi kutokuwa huru na haki na kwamba jambo hilo linachangiwa na NEC kutokuwa na nguvu ya kuwashughulikia watendaji wa Serikali.

“NEC ina changamoto ya kusimamia uchaguzi na ina watendaji wachache ukilinganisha na wakurugenzi wanaosimamia uchaguzi na kutangaza matokeo. Kama akihakikishiwa ulinzi anamtangaza asiye mshindi na hii ni changamoto kubwa sana kwa tume yetu,” alisema Kambaya.

Kampeni Siha

Jana, katika kampeni za uchaguzi Siha zilizofanyika viwanja vya Ngarenairobi, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alimpigia debe Dk Mollel akitaka wananchi wamchague ili akashirikiane kwa karibu na Serikali kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni migogoro ya ardhi, miundombinu mibovu ya barabara, ukosefu wa kituo cha afya na ukosefu wa ajira.

“Mkitupa Dk Mollel, lazima turudi hapa kushughulikia tatizo la ardhi ambalo limewafanya kuishi kwa msongamano wakati mmezungukwa na maheka ya ardhi,” alisema Polepole na kuongeza,

“CCM hatubebi mizigo ya misumari, tunapokea watu ambao ni vichwa na wanaweza kushirikiana na Serikali kuwaletea wananchi maendeleo.”

Kwa upande wake, Dk Mollel aliwaambia wananchi wa Ngarenairobi kuwa anatambua mchango wao wa mwaka 2015, hivyo wamrudishe ulingoni ili akatatue changamoto zinazowakabili ambazo alishindwa kuzitatua akiwa upinzani.

Kinondoni pingamizi kibao

Katika Jimbo la Kinodnoni, wagombea watatu wa Chadema, CCM na Sau waliwekeana pingamizi.

Msimamizi msaidizi wa jimbo hilo, Latifa Almas aliwataja wagombea hao kuwa ni Mtulia, Mwalimu na Johnson Mwangosi (Sau).

Almas alisema pingamizi la kwanza ni lile la Mwalimu alilomuwekea Mtulia, la pili ni la Mtulia kumwekea Mwangosi na la mwisho ni la mgombea wa CUF, Rajab Salum Juma kumuwekea Mwalimu.

Almasi alisema wagombea hao wote wameshapewa taarifa za pingamizi hizo, tayari wameshachukua fomu za kutakiwa kujieleza wanazotakiwa kuzijaza na kuzirejesha haraka iwezekanavyo.

Alisema iwapo waliowasilisha mapingamizi hao hawataridhika, wanaweza kukata rufaa NEC.

Wakili wa Mwalimu, Fredirick Kihwelo alisema pingamizi dhidi ya mgombea wa CCM ni kutofanya mrejesho wa gharama za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alisema nyingine ni Mtulia kushindwa kukidhi matakwa ya kisheria kwa kutojaza kwa usahihi fomu zake, kwa madai kuwa zimepigwa muhuri wa katibu wa CCM badala ya muhuri wa chama hicho tawala.

Alisema hoja ya mwisho ni Mtulia kujaza fomu akieleza kuwa anajishughulisha na kilimo cha mbogamboga, jambo ambalo Kihwelo amesema si kweli.

Hata hivyo, Mtulia alizijibu hoja hizo akisema ”Hili jambo jepesi sana na nimeandika ninachokijua na hakuna pingamizi hapo.”

Katika pingamizi la Mwalimu dhidi ya mgombea wa Sau, amesema Mwangosi amekosea kujaza fomu kwa maelezo kuwa jina lake linasomeka Mwangosi Johnson Joel badala Joel Johnson Mwangosi kama alivyoandika katika fomu ya kiapo.



Imeandikwa na Ibrahim Yamola na Bakari Kiango (Dar) na Flora Temba (Siha) 
Mwananchi

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.