AGPAHI YAKABIDHI KOMPYUTA 46 KWA AJILI YA VITUO VYA TIBA NA MATUNZO KWA WATU WANAOISHI NA VVU MKOA WA MARA


Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) limekabidhi kompyuta 46 zenye thamani ya shilingi milioni 70.2 zitakazotumika katika vituo vya tiba na matunzo (CTC) kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) kwenye halmashauri za wilaya mkoani Mara.
Shirika hilo limekabidhi kompyuta hizo siku ya Jumatatu, Januari 22, 2018 kwa Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Raphael Nyanda katika ukumbi wa mikutano wa Mwembeni uliopo katika Manispaa ya Musoma.

Akizungumza wakati wa kukabidhi kompyuta hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa alisema kompyuta hizo zitatumika kuhifadhi takwimu za wateja katika vituo vya tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na kusaidia upatikanaji wa taarifa kwa haraka na kwa usahihi zaidi.

“Leo tunayo furaha kukabidhi kompyuta 19 ambayo ni nyongeza ya kompyuta 27 ambazo zimeshapelekwa kwenye vituo vya afya hivyo hadi sasa tutakuwa tumekabidhi jumla ya kompyuta 46 tulizokabidhi kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu tuanze kutekeleza miradi ya Ukimwi katika mkoa wa Mara”, alieleza Dk. Sekela.

“Mbali na kukabidhi kompyuta pia tumefanikisha ajira kwa makarani takwimu "Data Clerks" 84 kwa halmashauri zote na tunawezesha upatikanaji wa mtandao wa intaneti kwa kutoa modem ili kurahisisha uingizaji wa takwimu katika mfumo wa kielektroniki na kutoa taarifa kwa wakati stahiki”,aliongeza Dk. Sekela.

Katika hatua nyingine alisema shirika hilo linatekeleza miradi ya Ukimwi katika vituo 112 vya kutolea huduma za afya mkoani Mara, kati ya vituo hivyo 67 ni vituo vya kutolea tiba na matunzo na 46 ni vya kutolea huduma ya kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT).

Dk. Sekela alibainisha kuwa katika kipindi cha mwezi Oktoba 2016 hadi Septemba 2017, jumla ya watu 182,712 mkoani humo walipata huduma ya upimaji wa VVU, kati yao wanaume walikuwa 51,868 (28%), watoto 31,423 (17%). Kati ya watu 182,712 waliopima, 7,325 (4%) waligundulika kuwa na maambuzi ya VVU na 6,022 (82%) walianzishiwa dawa za kupunguza makali ya VVU.

Aliongeza kuwa katika kipindi hicho pia akina mama wajawazito 49,937 walipima VVU , kati yao 981 sawa na 2% waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU na 755 sawa na 77% walianzishiwa dawa za kupunguza makali ya VVU.

Akipokea kompyuta hizo, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Raphael Nyanda alilishukuru shirika la AGPAHI kwa kutoa msaada huo na kuzitaka halmashauri za wilaya kuzitunza ili zidumu.

“Tunawashukuru sana AGPAHI na Watu wa Marekani kwa kuendelea kutushika mkono katika sekta afya, mwaka huu mmetuongeza shilingi bilioni 7.2 kwenye bajeti ya mkoa kwa ajili ya masuala ya Ukimwi, kwa kweli mmekuwa wadau wakubwa wa afya, naomba tuendelee kushirikiana kuwahudumia wananchi”, alieleza Nyanda.

“Serikali ya mkoa itasimamia vizuri fedha hizi,wakurugenzi tumieni fedha za wafadhili kwa malengo yaliyokusudiwa, msihamishe fedha, pia tuache tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na watendaji hakikisheni mnatoa takwimu sahihi", alisema Nyanda.

Mbali na kukabidhi kompyuta, Shirika la AGPAHI pia linaendesha mafunzo ya siku mbili kuhusu taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za wafadhili ambao ni Watu wa Marekani kupitia Centres for Disease Control (CDC) yaliyohudhuriwa na wakurugenzi na viongozi wa timu za afya za mikoa na wilaya.

Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya wanaojengewa uwezo ni kutoka Mji wa Bunda,Tarime Mji, Manispaa ya Musoma, Bunda Vijijini, Butiama, Musoma Vijijini, Rorya,Tarime na Serengeti na timu za afya za mkoa na wilaya kuhusu namna ya kutumia fedha za mfadhili sawa sawa na matakwa na makubaliano kati ya AGPAHI na serikali ya Marekani.

Mwaka huu shirika limetoa shilingi bilioni 7.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Ukimwi mkoani Mara ikiwa ni mara sita zaidi ya fedha iliyotolewa na shirika hilo mwaka 2016/2017 ambayo ilikuwa shilingi bilioni 1.1.

Shirika la AGPAHI linatekeleza miradi ya Ukimwi katika mikoa sita nchini ambayo ni Shinyanga, Simiyu, Geita,Mwanza, Tanga na Mara likishirikiana na serikali ya Tanzania kwa ufadhili wa serikali ya Watu wa Marekani kupitia CDC katika kutekeleza mradi wa “Boresha” ambao unatoa huduma za kinga, tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na Ukimwi.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mgeni rasmi, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Raphael Nyanda akizungumza wakati wa zoezi la makabidhiano ya kompyuta na kufungua mafunzo ya taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za wafadhili katika ukumbi wa mikutano wa Mwembeni manispaa ya Musoma.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Raphael Nyanda akilishukuru shirika la AGPAHI kwa kuipatia serikali ya mkoa wa Mara shilingi bilioni 7.2 kwa ajili ya miradi ya Ukimwi.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa akizungumza wakati wa kukabidhi kompyuta 46. Kushoto ni Meneja wa Shirika la AGPAHI Kanda ya Ziwa, Dk. Nkingwa Mabelele. Kulia ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Raphael Nyanda.
Dk. Sekela alisema kompyuta hizo zitatumika kuhifadhi takwimu za wateja wa CTC katika vituo vya afya na kusaidia upatikanaji wa taarifa kwa haraka na kwa usahihi zaidi.
Dk. Sekela akizungumza wakati wa kukabidhi kompyuta hizo.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Mara, Dk. Francis Mwanisi akilishukuru shirika la AGPAHI kwa msaada wa kompyuta 46.
Maboksi yenye kompyuta zilizotolewa na shirika la AGPAHI kabla ya kukabidhiwa kwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoani Mara.
Katikati ni Dk. Sekela akionyesha moja kati ya kompyuta 46 zilizotolewa na shirika la AGPAHI. 
Dk. Sekela akielezea zaidi kuhusu kompyuta hizo.
Dk. Sekela na Kaimu Katibu Tawala, Raphael Nyanda wakikabidhi kompyuta kwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Rorya Charles Kitamuru Chacha (aliyevaa nguo nyeusi kushoto) aliyeambatana na timu ya afya ya halmashauri hiyo.
Makabidhiano kwa viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Butiama yakiendelea.
Viongozi wa halmashauri ya Manispaa ya Musoma wakiongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Fidelica Myovela (aliyeshika boksi la kompyuta) wakipokea kompyuta.
Zoezi la makabidhiano ya kompyuta likiendelea.
Viongozi wa timu za afya za mikoa na wilaya wakiwa ukumbini.
Mratibu wa AGPAHI mkoa wa Mara, Alio Hussein akielezea lengo la mafunzo ya taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za wafadhili ambao ni Watu wa Marekani kupitia Centres for Disease Control (CDC).
Alio Hussein alisema shirika hilo linatekeleza miradi ya Ukimwi kwenye halmashauri 9 za wilaya mkoani Mara.
Afisa Ruzuku Mwandamizi wa shirika la AGPAHI, Leticia Gilba akitoa mada kuhusu vigezo na masharti ya mkataba wa utekelezaji wa Mradi wa Boresha mkoani Mara unaofadhiliwa na Watu wa Marekani kupitia CDC.
Leticia Gilba akiendelea kutoa mada ukumbini. 
Leticia Gilba akielezea kuhusu sheria na taratibu za matumizi ya fedha za wafadhili.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Rorya, Charles Kitamuru Chacha akichangia mada wakati wa mafunzo hayo.
Mratibu wa Ukimwi wa halmashauri ya wilaya ya Musoma, Mwanaidi Francis akichangia hoja wakati wa majadiliano ukumbini.
Kaimu Mganga Mfawidhi hospitali teule ya wilaya ya Rorya, Dk. Baraka Malegesi akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo.
Picha ya pamoja - wafanyakazi wa AGPAHI, wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na timu za afya za mkoa na wilaya. 
Picha ya pamoja.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.