MCHUNGAJI MASHIMO AHUKUMIWA KWENDA JELA MIAKA MIWILI



MAHAKAMA ya Wilaya Kinondoni, Dar es Salaam, imemhukumu mchungaji Daud Nkuba almaarufu Komando Mashimo, Nabii Nikaya, (Mchungaji Mashimo) kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia katika makosa mawili, kuingia kijinai katika ardhi isiyo yake na kuharibu mali.

Hukumu hiyo imetolewa Machi 18, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira, aliyesikiliza kesi hiyo, baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka ambao umethibitisha mashitaka hayo bila kuacha mashaka yoyote

Katika hukumu hiyo Komando Mashimo pia ameamriwa kulipa fidia ya Tsh milioni 5 huku Mahakama hiyo ikomuachia huru kwenye shtaka la kutishia kwa vurugu baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha shtaka hilo la kutishia kwa vurugu kama walivyomshitaki.

“Mshtakiwa katika kosa la kuingia kwa jinai mahakama inakupa adhabu ya kwenda jela miezi sita, kosa la kuharibu mali mahakama inakutia hatiani na kukupa adhabu ya kwenda jela miaka miwili pia mahakama inakuachia huru kwa kosa la kutishia kwa vurugu kwasababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi yako, hivyo utatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani”—amesema Hakimu Rugemalila.

Mbali na kifungo hicho, Mchungaji Mashimo pia atalazimika kulipa faini ya shilingi milioni 5.

Post a Comment

0 Comments