
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuwaunganishia maji wananchi watakaonufaika na Mradi wa Maji wa Bangulo kwa ufanisi na uaminifu, na kuhakikisha hakuna mianya yoyote ya rushwa itakayojitokeza kwani kuunganishiwa maji ni haki ya msingi ya mwananchi.
Waziri Aweso ameyasema hayo Jumanne, Machi 18, 2025, alipotembelea mradi huo uliopo mtaa wa Bangulo Hali ya Hewa, katika kata ya Pugu Station, wilayani Ilala, mkoani Dar es Salaam. Mradi huo unatarajiwa kunufaisha wananchi 450,000 wa kata mbalimbali za wilaya hiyo na wilaya jirani.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amewaomba wananchi wa Bangulo kutunza vyema miundombinu ya maji katika eneo lao na kutoa taarifa pindi watakapoona dalili ya kuvuja kwa maji, kutokana na baadhi ya mabomba katika eneo hilo kuwa ya muda mrefu.
Amesema kwa kufanya hivyo, upotevu wa maji utadhibitiwa na huduma kwa wananchi itaendelea kutolewa kwa ufanisi.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama, amesema mradi huo umegharimu jumla ya Shilingi bilioni 36.8, ikiwa ni pamoja na gharama ya ujenzi pamoja na usimamizi wa mradi, ambapo kwa ujenzi pekee gharama ni Shilingi bilioni 35.0, na usimamizi wa mradi ni Shilingi bilioni 1.8.
0 Comments