Mkuu wa wilaya ya Kahama,Frank Nkinda akiongea kabla ya kukabidhiwa kombe kwa mshindi na zawadi kwa timu zilizoshiriki
Mwakilishi wa Meneja Mkuu wa Barrick Bulyanhulu Chrispin Ngwaji akiongea kabla ya kukabidhiwa zawadi
Kakola FC
***
TIMU ya Kakola FC, imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Soka ya Kombe la Mahusiano “Mahusiano Sports Bonanza Cup” baada ya kuichapa timu ya Ng’wasabuka mabao 3-0 katika mchezo wa fainali na kubeba kombe la ushindi pamoja na zawadi Mbalimbali .
Mechi ya fainali hiyo iliyokuwa na ushindani mkali ilichezewa kwenye uwanja wa shule ya msingi Kakola, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala na kuhudhuriwa na watazamaji wengi wakiwemo viongozi mbalimbali wa Serikali na Wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick Bulyanhulu ambao umeandaa na kudhamini mashindano hayo.
Mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda alishirikiana na Mwakilishi wa Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Chrispin Ngwaji ambao mbali na kukabidhi kombe la ushindi kwa Kakola FC, pia walikabidhi zawadi mbalimbali ikiwemo ng’ombe.
Katika mchezo huo wa fainali ambao ulishuhudiwa na mamia ya washabiki wa soka walionekana kufurahia fainali hiyo kutokana na timu zote mbili kutumia kasi, mbinu na akili wakati wa mchezo huo.
Akiongea baada ya kumalizika mechi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Frank Nkinda, ameushukuru Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa kuandaa Bonanza hilo ambalo limewezesha vijana kupata fursa ya kuonesha vipaji vyao kwa jamii na wadau mbalimbali wa michezo pia mashindano hayo yamekuwa jukwaa la kujenga uhusiano mzuri baina ya mgodi na jamii iliyouzunguka.
Naye Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu Chrispin Ngwaji amesema Bonanza hilo lilishirikisha timu 16 kutoka katika kata 3 za Bugarama, Bulyanhulu na Mwingiro na mbali na zawadi kwa timu iliyoibuka bingwa kila timu shiriki imepatiwa zawadi ya Jezi na mpira.
Amesema Mgodi wa Barrick Bulyanhulu utaendelea kuandaa mabonanza kama haya katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha sekta ya michezo mbalimbali nchini na kukuza vipaji vya vijana.
Mashindano ya Kombe la Mahusiano yalizinduliwa June 14, mwaka huu na yaliandaliwa na kudhaminiwa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu yakiwa na kauli mbiu inayosema “Umoja na Furaha kwa jamii ya Bulyanhulu,piga mpira jenga mahusiano” Na yamelenga kukuza uhusiano mzuri kati ya Mgodi na jamii inayozuguka mgodi huo.
Aidha, mashindano hayo yamesaidia kuongeza uelewa juu ya fursa mbalimbali zilizopo mgodini na wananchi kuelewa miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na mgodi huo katika maeneo yao kwa ajili ya kuwaletea maendeleo.


0 Comments