Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, akizungumza na wananchi wakati wa kukagua eneo la ujenzi wa Shule ya Sekondari Kalo kabla ya kukabidhi Sh. milioni 603.8 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Ushetu, Emmanuel Malima, akieleza hatua za utekelezaji wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kalo baada ya kupokelewa kwa fedha za Sh. milioni 603.8.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, akizungumza na wananchi wakati wa ukaguzi wa eneo litakalojengwa Shule ya Sekondari Kalo katika Kata ya Ulewe.
Diwani wa Kata ya Ulewe, Mhe. Kulwa Emmanuel, akizungumza na wananchi wakati wa hafla ya kukabidhi fedha za ujenzi wa Shule ya Sekondari Kalo.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, amekabidhi rasmi shilingi milioni 603.8 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Kalo iliyopo Kata ya Ulewe, akisisitiza kuwa kuanzia sasa hakuna mwananchi atakayechangishwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.
Akizungumza Julai 21, 2026, baada ya kukagua eneo la ujenzi wa Shule ya Sekondari Kalo na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Ulewe, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, amesema fedha hizo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi, kuongeza fursa za watoto kupata elimu ya sekondari na kuboresha mazingira ya kujifunzia nchini.
"Hapa mliomba shule ya sekondari, mkaandaa maombi na muhtasari, nami nikawaahidi kuwa nitawaunga mkono. Leo nimetimiza ahadi hiyo kwa kuwaletea shilingi milioni 603.8 zilizotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa shule hii," amesema Cherehani.
Mbunge huyo amewataka viongozi wa Halmashauri na kamati za ujenzi kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa uadilifu na kwa malengo yaliyokusudiwa ili kupata majengo yenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya elimu.
"Fedha hizi zitumike kama zilivyokusudiwa. Hakikisheni majengo yanajengwa kwa ubora. Endapo kutakuwa na fedha zitakazobaki, zielekezwe kwenye miundombinu mingine ya shule badala ya kugawana. Baneni matumizi ili kuwapunguzia wananchi mzigo na tujue matumizi halisi ya kila shilingi," amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Cherehani ametangaza rasmi kusitishwa kwa michango iliyokuwa inaendelea ya wananchi kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo, akieleza kuwa Serikali tayari imechukua jukumu hilo.
"Kuanzia leo pasiwe na mchango wa wananchi kwa ajili ya shule hii. Yale mabati 96 pamoja na shilingi milioni tatu zilizokuwa zimekusanywa zihamishiwe kwenye ujenzi wa Zahanati. Mimi pia nitaongeza shilingi milioni tano ili kuanzisha ujenzi wa zahanati," amesema.
Aidha Cherehani, ameagiza taratibu zote za umiliki wa eneo la shule zikamilishwe kwa haraka ili hati ya eneo isajiliwe kwa jina la Shule ya Sekondari Kalo, sambamba na kuhakikisha mchakato wa kukabidhiana kati ya shule ya msingi na sekondari unafanyika kwa kufuata sheria na taratibu ili kuepusha migogoro ya baadaye.
Mbunge huyo pia ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya barabara kwa kujenga madaraja na kusimamia uhamishaji wa baadhi ya barabara kwenda chini ya usimamizi wa TARURA na TANROADS ili kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri na uchukuzi katika Jimbo la Ushetu.
Akizungumza kuhusu ustawi wa wananchi, Cherehani amewataka wakazi wa Ushetu kuendelea kushikamana na kufanya kazi kwa bidii ili kujenga uchumi imara wa familia na jamii, huku akiwataka waendesha bodaboda kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazogharimu maisha ya vijana.
"Nataka tuijenge Ulewe na Ushetu yenye wananchi wenye uchumi mzuri. Tufanye kazi, tushirikiane na tupendane. Waendesha bodaboda endesheni pikipiki kwa uangalifu, tusiendelee kupoteza vijana wetu kwa ajali zinazoweza kuzuilika," amesema.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Ushetu, Emmanuel Malima, amesema tayari fedha hizo zimepokelewa na maandalizi ya ujenzi yameanza, huku matarajio yakiwa ni kuona shughuli kubwa za ujenzi zikianza kabla ya mwezi Agosti mwaka huu.
Amefafanua kuwa kiasi cha shilingi milioni 603.8 kitagharamia ujenzi wa madarasa nane, jengo la utawala, vyumba vitatu vya maabara, maktaba, chumba cha kompyuta pamoja na matundu 16 ya vyoo, yakiwemo manane ya wavulana na manane ya wasichana.
Malima amesema lengo la Halmashauri ni kuhakikisha Shule ya Sekondari Kalo inakamilika, inasajiliwa na kuanza kupokea wanafunzi katika mwaka ujao wa masomo.
Naye Diwani wa Kata ya Ulewe, Mhe. Kulwa Emmanuel, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha za maendeleo katika kata hiyo pamoja na kumpongeza Mbunge Emmanuel Cherehani kwa juhudi zake za kusimamia upatikanaji wa miradi ya maendeleo, akieleza kuwa hatua hiyo itaondoa adha ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu kutafuta elimu ya sekondari.
Wananchi wa Ulewe wameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa ahadi hiyo, wakisema ujio wa fedha hizo ni ishara ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuboresha huduma za elimu na kuharakisha maendeleo katika maeneo ya vijijini.
0 Comments