
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema wimbi la joto lisilo la kawaida linaloikumba Ulaya huwenda limesababisha vifo vya ziada vya zaidi ya watu 1,300 tangu Juni 21.
Rekodi za viwango vya joto zimeendelea kuvunjwa katika mataifa kadhaa ya Ulaya, yakiwemo Ujerumani, Poland na Jamhuri ya Czech, huku wimbi hilo la joto kali likiendelea kuelekea mashariki mwa bara hilo.
Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Tedros alisema joto kali mara nyingi huitwa "muuaji kimya" kwa sababu linaweza kusababisha vifo bila dalili za wazi.
Aliongeza kuwa nyumba, maeneo ya kazi na shule nyingi barani Ulaya hazikujengwa kuhimili viwango hivyo vya juu vya joto.
Wizara ya Afya ya Ufaransa imesema takriban vifo 1,000 zaidi ya vilivyotarajiwa vimerekodiwa nchini humo tangu Jumatano, huku idadi kubwa ya vifo hivyo ikiwa ni ya watu wenye umri wa miaka 65 na kuendelea.
WHO imeonya kuwa Ulaya ndiyo bara linaloongezeka joto kwa kasi zaidi duniani, kwa kiwango cha mara mbili ya wastani wa ongezeko la joto duniani.
"Mamilioni ya watu barani Ulaya kwa sasa wanaishi chini ya wimbi kali la joto, mamia wamefariki, shule zimefungwa na mifumo ya usambazaji umeme iko chini ya shinikizo kubwa," alisema Tedros.
0 Comments