Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani (katikati), akitembelea na kukagua eneo la ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Isanga katika Kata ya Idahina, Julai 20, 2026, ili kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa zaidi ya Shilingi milioni 603.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani (wa pili kulia), akitembelea na kukagua eneo la ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Isanga katika Kata ya Idahina, Julai 20, 2026, ili kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa zaidi ya Shilingi milioni 603.

Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Isanga, Kata ya Idahina, kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Isanga.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Isanga, Kata ya Idahina, kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Isanga. Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Isanga, Kata ya Idahina, akiuliza kuhusu utaratibu wa kupata mikopo inayotolewa na Halmashauri wakati wa mkutano wa hadhara ulioongozwa na Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, Julai 20, 2026.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, akizungumza na wananchi wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero, maoni na mapendekezo yao kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kijiji cha Isanga, Kata ya Idahina, Julai 20, 2026.
Wananchi wa Kijiji cha Isanga, Kata ya Idahina, wakifuatilia kwa makini mkutano wa hadhara ulioongozwa na Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani
Wananchi wa Kijiji cha Isanga, Kata ya Idahina, wakipiga picha ya kumbukumbu pamoja na Mbunge wao, Mhe. Emmanuel Cherehani, baada ya mkutano wa hadhara uliolenga kusikiliza kero za wananchi na kutoa mrejesho kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Julai 20, 2026.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mkoani Shinyanga, Mhe. Emmanuel Cherehani, amesema hakuna mwananchi atakayechangishwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Isanga katika Kata ya Idahina, akieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imetoa Shilingi 603,890,563 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Mhe. Cherehani ameyasema hayo leo Julai 20, 2026 alipokagua eneo la ujenzi wa shule hiyo na kukabidhi fedha za utekelezaji wa mradi huo, huku akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Isanga.
Amesema fedha hizo zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ambayo itakuwa shule ya pili ya sekondari ndani ya Kata ya Idahina, hatua inayolenga kuongeza fursa za elimu na kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Idahina.
Amesema fedha zilizotolewa na Serikali zinatosha kuanza utekelezaji wa mradi huo, hivyo hakuna sababu ya wananchi kuombwa michango ya fedha, bali wanapaswa kushiriki katika shughuli za maendeleo na kusimamia maendeleo ya eneo lao.
"Nimewaletea shilingi milioni 603 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Isanga, Hakuna mwananchi atakayeombwa fedha. Namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha hizi za maendeleo," amesema Mhe. Cherehani.
Mbunge huyo amewaomba wasimamizi wa mradi huo kuwa waadilifu, waaminifu na kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili ujenzi wa shule hiyo ukamilike kwa ubora na kuwanufaisha wananchi wa Kata ya Idahina.
Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta za elimu na afya ndani ya Jimbo la Ushetu, ambapo mbali na ujenzi wa shule, imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati ili kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi.
Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa ataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha huduma za afya zinaimarika zaidi, ikiwa ni pamoja na kuendelea kufuatilia upatikanaji wa gari la kubebea wagonjwa (ambulance) kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Katika kuhimiza ustawi wa familia na maendeleo ya kiuchumi, Cherehani amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii, kutafuta kipato halali na kutumia mali zao kwa manufaa ya familia.
"Wananchi tusaidieni kufanya kazi. Tafuteni pesa, tunzeni familia zenu. Baraka zote mnazolima na mnazochimba zinatokana na wake zenu, hivyo tumieni mali pamoja na familia zenu. Nataka niongoze watu wenye uchumi imara," amesema.
Mbunge huyo pia ametangaza kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuboresha miundombinu ya barabara, akieleza kuwa barabara ya Mwabomba–Kaliua itajengwa kwa kiwango cha lami huku akisisitiza kuwa anaendelea kufuatilia ujenzi na ukarabati wa barabara mbalimbali katika jimbo hilo.
Kuhusu changamoto za wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Kigosi, amesema Serikali inaendelea kutafuta suluhisho la kudumu ikiwemo kufanya maboresho ya sheria ili kuwezesha wananchi kutengewa maeneo ya malisho kwa utaratibu unaokubalika.
Akizungumzia huduma za usajili wa vitambulisho vya taifa, Cherehani amesema maafisa wa NIDA watakwenda Kata ya Idahina kwa ajili ya kuandikisha wananchi wapya pamoja na kurekebisha taarifa za waliokwisha kujiandikisha.
Katika hatua nyingine, amewataka watendaji wa kata kuhakikisha wanasoma hadharani taarifa za mapato na matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo ili wananchi wajue namna fedha zinavyotumika.
"Tukisoma mapato na matumizi, hatutakuwa na kelele. Wananchi wataelewa maendeleo ya michango na fedha zinazotolewa na Serikali," amesisitiza.
Amesema ziara zake za kupita kijiji kwa kijiji ni sehemu ya kuwashukuru wananchi kwa imani waliyoonyesha kwake katika uchaguzi na pia kusikiliza changamoto zao ili kuzitafutia ufumbuzi.
Awali akisoma taarifa ya Kata ya Idahina kwa niaba ya Mtendaji wa Kata, Mwalimu Godfrey Biashara amesema kata hiyo ina vijiji vitano na wakazi 26,902, ikiwa na shule za msingi 11 na shule moja ya sekondari ya Idahina, huku shule zote zikikabiliwa na upungufu wa walimu.
Amesema Serikali imetoa Shilingi milioni 90 kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Idahina na zaidi ya Shilingi milioni 603 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Isanga, mradi unaotarajiwa kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuongeza fursa za elimu kwa vijana wa kata hiyo.
Aidha, ameeleza kuwa ujenzi wa zahanati katika vijiji mbalimbali unaendelea pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya Mwabomba, huku changamoto kubwa zilizobaki zikiwa ni miundombinu ya barabara na madaraja pamoja na upungufu wa walimu.
Naye Diwani wa Kata ya Idahina, Mhe. Mathias Makashi, Makashi, ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa Shule ya Sekondari Isanga, akisema mradi huo utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Idahina na kuongeza fursa za vijana kupata elimu katika mazingira bora.
Aidha amempongeza Mbunge Cherehani kwa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisema wananchi wameendelea kumuunga mkono kutokana na matokeo ya kazi yake.
"Tumeng'ang'ana na Cherehani kwa sababu anatuletea maendeleo. Ujenzi wa madaraja, vituo vya afya na shule unaonekana. Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Mbunge wetu imeleta maendeleo makubwa. Mbunge wewe ni wetu, endelea kutupigania, sisi tutamalizia kufunga magoli. Tangu dunia iumbwe, Mbunge huyu amevunja rekodi kwa kutuletea maendeleo," amesema diwani huyo.
0 Comments