WANANCHI SHINYANGA WATOA MAONI RASIMU YA MKATABA WA HUDUMA ZA SHUWASA, WAPENDEKEZA MITA ZA PRE -PAID

  

Mkurugenzi wa Shuwasa Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Wananchi wa Manispaa ya Shinyanga wamependekeza kuanzishwa kwa mita za malipo ya kabla (prepaid water meters) ili kudhibiti malalamiko ya bili kubwa za maji, wakati wakisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa huduma bora ya majisafi na usafi wa mazingira.

Mapendekezo hayo yametolewa leo Machi 26, 2026, katika mkutano wa wadau wa maji ulioandaliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga kwa lengo la kujadili rasimu ya mkataba mpya wa huduma kwa wateja.

Mmoja wa wananchi hao, Ashirafu Said amesema licha ya maboresho yanayoendelea kufanywa na SHUWASA, bado kuna changamoto ya malalamiko ya bili zisizoendana na matumizi halisi ya maji.
“Tunapongeza juhudi za SHUWASA, lakini tunaomba kuanzishwa kwa mita za malipo ya kabla ili kuongeza uwazi. Kama ilivyo kwenye umeme wa LUKU, tokeni ikiisha huduma inakatika, hivyo kuepusha bili kubwa zisizoeleweka,” amesema Ashirafu.

Mgeni rasmi katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ameitaka SHUWASA kuhakikisha huduma wanazotoa zinaendana na matakwa ya mkataba wa huduma kwa wateja pamoja na kuzingatia miongozo ya kisheria.

Amesisitiza umuhimu wa kushughulikia kwa wakati changamoto za wananchi ili kuongeza imani na kuridhika kwa wateja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, amesema mkataba uliopita umefikia tamati, na sasa mamlaka hiyo ipo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha rasimu ya mkataba mpya utakaodumu kwa miaka mitatu (2026–2029).
Amefafanua kuwa mkataba huo utaanza kutumika rasmi baada ya kupitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, na kwamba unaweka wazi haki na wajibu wa pande zote mbili ,mtoa huduma na mteja kwa lengo la kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa huduma.

Kuhusu mita za malipo ya kabla, Mhandisi Katopola amesema utekelezaji wake utafanyika kwa awamu kutokana na gharama zake kuwa kubwa ikilinganishwa na mita za kawaida.

Ameongeza kuwa katika hatua ya awali, mita hizo zitaanza kufungwa kwenye maeneo yenye changamoto ya ulipaji wa bili, hususan vituo vya umma vya kuchotea maji, huku zoezi hilo likitarajiwa kuanza mwezi Aprili 2026.
Naye Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa SHUWASA, Rueben Mwandumbya, akiwasilisha rasimu ya mkataba huo, ameeleza kuwa mamlaka ina wajibu wa kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama ya kutosha kwa viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, pamoja na kutoa huduma bora za usafi wa mazingira.

Ameainisha majukumu mengine kuwa ni pamoja na kulinda vyanzo vya maji, kutoa elimu kwa wateja kuhusu sera ya taifa ya maji, kuhimiza ulipaji wa bili kwa wakati, kushughulikia malalamiko ya wateja kwa haraka, pamoja na kudhibiti upotevu wa maji na kutunza kumbukumbu sahihi za wateja.

Aidha, amesema SHUWASA ina haki ya kulipwa gharama halali za huduma, kusitisha huduma kwa wateja wanaoshindwa kulipa bili ndani ya siku 30, na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waharibifu wa miundombinu na wezi wa maji.

Kwa upande wa wateja, ameeleza kuwa wanapaswa kulipa bili kwa wakati, kutoa ushirikiano kwa watumishi wa mamlaka, kutoa taarifa sahihi kuhusu vitendo vya rushwa na wizi wa maji, pamoja na kulinda vyanzo vya maji na kuhudhuria mikutano ya wadau ili kupata taarifa muhimu.

MAELEZO KATIKA PICHA
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza.

Mkurugenzi wa huduma kwa wateja kutoka SHUWASA Rueben Mwandumbya akiwasilisha mkataba wa huduma kwa wateja.
Mwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA Ruben Kitinya akizungumza.


Picha na Marco Maduhu 

Post a Comment

0 Comments