
Mkurugenzi Mtendaji wa YOGE, Wakili Philomena Mwalongo
***
Na Mwandishi Wetu, Songea
Serikali mkoani Ruvuma imeshauriwa kuzuia kabisa uingizwaji wa makundi makubwa ya mifugo mkoani humo ili kunusuru nchi dhidi ya janga la njaa, kwa kuzingatia kuwa Ruvuma ni moja ya mikoa muhimu kwa uzalishaji wa chakula nchini.
Wito huo umetolewa na Shirika la Youth Environmental Justice and Gender Equality (YOGE) mwishoni mwa wiki, ikiwa ni sehemu ya mapendekezo yaliyotolewa katika kikao kazi kilichowakutanisha watunga sera mkoani humo kupitia mradi wa Sauti za Maji.
Akiwasilisha mapendekezo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa YOGE, Wakili Philomena Mwalongo, amesema mradi huo umebaini kuwepo kwa tishio la uvamizi wa makundi makubwa ya mifugo, jambo linalohatarisha uendelevu wa Bonde la Ruvuma.
Ameeleza kuwa ardhi ya mkoa huo ni tepefu na inafaa zaidi kwa shughuli za kilimo kuliko ufugaji wa mifugo mingi.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa ni pamoja na kuendesha kampeni endelevu za upandaji wa miti rafiki kwa mazingira, kuhifadhi vyanzo vya maji, pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia majukwaa mbalimbali kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na rasilimali za maji.
Akichangia katika kikao hicho, mkulima kutoka Matogoro, eneo lililo chanzo cha Mto Ruvuma, Fatuma Gawaza, amesisitiza umuhimu wa wanawake na vijana kuwezeshwa kupata mikopo ili wanunue pampu na mabomba ya umwagiliaji, hatua itakayowasaidia kuachana na kilimo kandokando ya mto.
Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo la Mbinga, Mhashamu John Ndimbo, amependekeza elimu ya mazingira ijumuishwe katika mitaala ya elimu kuanzia shule za msingi hadi elimu ya juu, ili kujenga kizazi chenye uelewa wa kutosha kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.
Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Louis Chomboko, ameipongeza YOGE kwa jitihada zake za kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na rasilimali za maji mkoani humo.
Ameahidi kuwa Serikali ya Mkoa itayafanyia kazi mapendekezo yaliyowasilishwa, ikiwemo kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama.
Mradi wa Sauti za Maji unatekelezwa na YOGE kwa kushirikiana na Tanzania Media for Community Development (TAMCODE) kwa ufadhili wa IUCN Bridge.
Mradi huo unalenga kuhamasisha ushiriki wa wanawake na vijana katika usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za maji na mazingira ndani ya Bonde la Ruvuma


















0 Comments