Na Rose Ngunangwa - Dar es salaam
Waandishi wa Habari wametakiwa kuchukua jukumu la kuripoti stori za mabadiliko ya tabia nchi badala ya kusubiri mafuriko yatokee ndipo wafanye hivyo.
Vilevile wameaswa kufanya uandishi wenye kujenga kwa kutoa taarifa za mabadiliko ya tabia nchi ili kuwawezesha watu kufanya maamuzi sahihi.
Catherine Mackie, Mhariri wa Mafunzo na Mawasiliano kutoka Thomson Foundation ametoa wito huo Machi 24,2025 wakati wa mdahalo wa wadau wa habari kuhusu kuripotia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi ulioandaliwa jijini Dar es Salaam na Baraza la Habari Tanzania kwa kushirikiana na Wajibika.
Catherine ambaye ni mwandishi wa zamani wa BBC na mwandishi wa Kitini cha Vyombo vya Habari kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi Tanzania amesema; mabadiliko ya tabia nchi ni jambo ambalo lipo na hivyo ni muhimu sauti zote zikasikika
" Vyombo vya habari havihitaji dawati maalumu la Mazingira. Kila mwandishi katika chombo cha Habari ni mwandishi wa Mazingira. Vyombo vya Habari vinatakiwa kusimulia stori kwa namna inayovutia," alisema Mackie.
Martha Fatael mwandishi kutoka Majira alisisitiza umuhimu wa kuanzisha mfuko maalumu wa mabadiliko ya tabia nchi ili kuwasaidia waandishi wa habari kukuza uelewa wa wananchi juu ya mabadiliko ya tabia nchi.
Mwandishi huyo ambae pia ni mnufaika wa mafunzo ya mabadiliko ya tabia nchi na kuripotia mkutano wa COP 30, alisisitiza kuwa watanzania walio wengi hususani vijijini wana uelewa mdogo wa mabadiliko ya tabia nchi huku baadhi yao wakiamini kuwa jambo hilo haliwahusu.
Mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa na athari nchiini Tanzania na kusababisha kuongezeka kwa joto, mvua zisizotabirika, upungufu wa maji na kutishia kilimo na anuwai.
















0 Comments