WANAUME TUPIMENI AFYA ZETU
John Francis Haule akipima afya
***
Kila ifikapo tarehe Mosi Desemba, dunia inaadhimisha Siku ya UKIMWI, ikiwa ni kumbukumbu ya kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa Virusi vya UKIMWI (VVU) na jinsi ya kuepuka maambukizi yake.
Maradhi haya, tangu yalipoanza kuikumba dunia, yameleta madhara makubwa kwa familia nyingi, yakisababisha vifo na kuharibu maisha ya watu wengi, baadhi yao wakiwa na ufahamu na wengine wakikumbwa na hali hii bila kujua.
Katika jamii zetu, ni vigumu kupata familia ambayo haijawahi kukutana na changamoto hii ya VVU, iwe kwa njia ya moja kwa moja au kupitia watu wa karibu. Katika historia ya nchi yetu, mgonjwa wa kwanza aliyejulikana na ugonjwa wa UKIMWI aligundulika mnamo mwaka 1980 katika mkoa wa Kagera. Wakati huo, ugonjwa huu ulikuwa ukijulikana kwa jina la Juliana – jina ambalo wahenga wengi wataendelea kulikumbuka.
Riwaya maarufu ya Passed Like a Shadow ya mwandishi Bernard Mapalala, inaelezea jinsi ugonjwa huu ulivyoharibu maisha ya watu wengi, akiwemo mhusika mkuu Adyeri, ambaye aliathirika na VVU. Hadi leo, licha ya juhudi kubwa za kuelimisha jamii, ugonjwa wa VVU unadhihirisha kuwa ni changamoto kubwa katika mapambano ya afya ya umma.
Kwa miaka mingi, elimu kuhusu VVU imekuwa ikitolewa kupitia njia mbalimbali ikiwemo mashuleni, semina, makongamano ya kijamii na kidini, na kwa ushirikiano na serikali, kupitia taasisi kama Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS). Serikali pia imeanzisha kamati maalum ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, jambo ambalo limeongeza uzito na umuhimu wa suala hili katika mipango ya taifa.
Katika awamu ya awali, ugonjwa wa UKIMWI ulikuwa hauna tiba, lakini kwa sasa kuna matibabu yanayoweza kupunguza athari za virusi hivi katika mwili, kupitia dawa za kufubaza virusi (ARVs). Dawa hizi zinapatikana bure katika hospitali zetu, na huduma za ushauri pia hutolewa bure. Upatikanaji wa dawa hizi umepunguza hofu miongoni mwa jamii, ingawa kuna baadhi ya watu bado wanaogopa kupima afya zao ili kutambua hali zao. Hivyo, ni muhimu kuhamasisha jamii kuendelea na tabia ya kupima afya ili kupunguza maambukizi.
VIRUSI VYA UKIMWI VINAAMBUKIZWA KWA NJIA HIZI:
1. Kujamiiana bila kutumia kinga (kondomu):
Hii ni njia kuu ya maambukizi ya VVU. Kujamiiana bila kutumia kondomu ni hatari kubwa, kwani hupeleka virusi kutoka kwa mtu mmoja mwenye maambukizi kwenda kwa mwingine.
2. Kutumia vifaa vyenye ncha kali vinavyoshirikishwa:
Maambukizi yanaweza kutokea kupitia matumizi ya vifaa kama vile wembe, sindano, au vifaa vya upasuaji vinavyotumika kwa watu wengi, ambapo mmoja wao anaweza kuwa na maambukizi ya VVU.
3. Kugusana na damu ya mtu mwenye maambukizi:
Maambukizi yanaweza kutokea kupitia kugusana na damu ya mtu mwenye maambukizi, hasa wakati wa ajali, kuongezewa damu au upasuaji ambapo damu inachanganywa.
4. Kupitia kupitishiwa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto:
Mama mjamzito mwenye maambukizi ya VVU anaweza kumwambukiza mtoto wake akiwa tumboni (kupitia plasenta), wakati wa kuzaliwa au wakati wa kunyonyesha. Hii ni njia ya maambukizi ambayo inahitaji udhibiti wa kiafya ili kupunguza hatari ya mtoto kuambukizwa.
5. Kupitia uhusiano wa damu:
Maambukizi yanaweza pia kutokea kupitia uhusiano wa damu kwa njia ya kushirikiana kwa karibu, kama vile kwenye mashindano ya michezo ambapo kuna uwezekano wa kumwagika kwa damu, au katika mazingira ya kazi ya afya ambapo inahitajika matumizi ya vifaa vya kinga.
6. Kupitisha virusi kwa njia ya mawasiliano ya kinywa na damu:
Ingawa si ya kawaida, VVU vinaweza kuambukizwa kwa njia ya mawasiliano ya kinywa na damu, hasa ikiwa kuna vidonda au majeraha kwenye kinywa cha mtu ambaye hajapata maambukizi.
Ni muhimu kuelewa kuwa VVU havienei kwa njia ya kupiga chafya, kukohoa, kugusa, kushikana mikono, au kutumia vyombo vya kawaida kama vikombe na vyombo vya kula.
Kwa hivyo, kujua njia hizi za maambukizi kunasaidia jamii kuchukua tahadhari na kuepuka hatari za kupata maambukizi ya VVU.
NAMNA YA KUEPUKA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI NA MARADHI YA SHABIHIANO
Maradhi kama kaswende, gonorea, na homa ya ini, yanapaswa kuepukwa kwa njia zifuatazo:
1. A - Abstinence (Acha kabisa ngono, hasa ngono zisizo na kinga).
2. B - Be faithful to your partner (Kuwa mwaminifu kwa mwenza wako).
3. C - Use condom during sexual intercourse (Tumia kondomu wakati wa kujamiiana).
Kuna umuhimu mkubwa wa kuwa waaminifu kwa wenza wetu, kwani miongozo ya dini na jamii inasisitiza kuwa ngono nje ya ndoa ni haramu. Wanaume, tunahitaji kuwa waaminifu na kuepuka tabia ya kuvunja ndoa kwa kushiriki katika ngono zembe. Viongozi wa dini wanatufundisha kuhusu hatari ya zinaa, na ni vyema tukazingatia maadili haya ili kuzuia maambukizi ya VVU na maradhi mengine yanayohusiana na ngono.
MADHARA YA KUTOPIMA AFYA
Kutopima afya kuna madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na:
- Kupunguza kinga ya mwili na kufanya mwili kuwa rahisi kushambuliwa na magonjwa mengine nyemelezi.
- Kulegeza uangalifu na kuongeza hatari ya vifo mapema.
- Kutokuwa na uhakika na hali ya afya yako, ambayo inaweza kuleta hofu na kushindwa kujipanga ipasavyo.
UMUHIMU WA KUPIMA AFYA
1. Kujitambua ili kujilinda dhidi ya maambukizi.
2. Kupunguza tabia hatarishi kama vile ngono zembe.
3. Kuepuka kuambukiza wengine na kuzuia maambukizi.
4. Kuanzisha matibabu mapema, ikiwa maambukizi yatatambulika.
5. Kusaidia serikali kupata takwimu sahihi ili kuboresha huduma za afya.
6. Kudumisha uhusiano mzuri kwa wenza na familia.
7. Kupunguza hofu na kuleta amani katika familia.
HITIMISHO
Methali ya Kiswahili isemayo "Mficha maradhi kifo humuumbua" ni ukweli usiopingika. Wanaume wengi hawana desturi ya kupima afya zao, hasa linapokuja suala la VVU, na mara nyingi tunaacha majibu ya afya yetu kwa wake zetu au familia ili tuweze kujua hali ya afya yetu. Wanaume, tunapaswa kuchukua hatua za haraka katika kupima afya zetu ili kujilinda na kuepuka hatari ya maambukizi.
Pia, tunahitaji kupunguza mipango ya kando, michepuko na ngono zisizo salama, ili kuepuka madhara. Ni muhimu kuchukua hatua ya kupima afya zetu ili kuhakikisha tunaishi maisha salama na yenye afya, tukijua kuwa UKIMWI wa leo si sawa na wa miaka ya 1980. Kwa sasa, matibabu yanapatikana na yanaweza kusaidia kudumisha afya nzuri, ikiwa hatua za mapema zitachukuliwa.
Kauli Mbiu:
"PIMA, JITAMBUE, ISHI"
Makala hi imeandikwa na:
John Francis Haule
Mkuu wa Soko Kuu la Arusha
Simu: 0756717987 au 0711993907
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: