KOCHA MPYA WA SIMBA NI HUYU
WAKATI makocha wawili waliowahi kuinoa Simba miaka kadhaa iliyopita Mserbia Milovan Cirkovic na Mcroatia Zdravko Logarusic ni miongoni mwa makocha 80 waliowasilisha wasifu wao (CV) kuitaka nafasi ya Mfaransa Didier Gomes aliyejiondoa mwenyewe, kocha mpya ajaye atalazimika kutimiza mambo kadhaa ili ajenge ngome yake ndani ya timu hiyo.
Kwanza ni lazima awe na leseni ya ukocha daraja A ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) au ile ya daraja la juu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA Pro) ambayo Gomes hakuwa nayo hali iliyosababisha azuiwe kuwepo kwenye benchi katika mechi za mashindano za CAF, taarifa za ndani Simba zimesema.
Kocha huyo mpya wa Simba pia anapaswa kujiandaa kutibu tatizo sugu la safu ya ulinzi ya timu hiyo kuwa na udhaifu wa kuokoa mipira ya juu ambayo ndio imechangia kwa kiasi kikubwa Simba kupoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy nyumbani na kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Mbali na hayo, mtihani mwingine kwa kocha mpya wa Simba ni kuirudishia makali yake ya kucheza soka la kuvutia na kufunga mabao kutokana na nafasi ambazo inatengeneza kutokana na pasi za chinichini badala ya kutegemea mipira iliyokufa na ile ya juu ambayo ndio imewapa idadi kubwa ya mabao msimu huu.
Kocha huyo pia ana kibarua cha kuimarisha kiwango na ubora wa mchezaji mmojammoja na kuandaa wachezaji watakaokuwa uti wa mgongo wa timu hiyo, kuziba nafasi za Clatous Chama na Luis Miquissone ambao walikuwa chachu ya ujenzi wa mashambulizi na mabao ya Simba hapo nyuma.
Mwanzo mbaya wa msimu, ikiwamo kutolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ni mambo yaliyochangia kuondoka kwa Gomes na mabosi wa klabu hiyo ya Msimbazi tayari wameingia mzigoni kuhakikisha wanampata kocha wa kurejesha tabasamu kwa mashabiki wao.ADVERTISEMENT
Gomes alijiunga na Simba Januari 24 mwaka huu akichukua nafasi Sven Vandenbroeck aliyefungashiwa virago baada ya wekundu hao kutofanya vizuri. Na baada ya Simba kufungwa 3-1 na Jwaneng Galaxy na kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, makocha walianza kutuma CV zao mara tu ilipotolewa taarifa ya kuondoka kwa Gomes.
Akizungumza na Mwanaspoti, mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, Mulamu Nghambi alisema jana walipokea CV za makocha wengi wakiwemo Cirkovic na Logarusic.
“Makocha wengi wametuma CV zao. Miongoni mwao hao wawili waliowahi kuifundisha Simba na wanaijua vilivyo, lakini bado hatujakaa na kuchambua nani anatufaa,” alisema Mulamu.
MAKOCHA WASAIDIZI
Mulam alitolea ufafanuzi wa kuondolewa kwa kocha wa viungo, Adel Zrane pamoja na wa makipa, Milton Nienov ambao ilielezwa kuwa hawana sifa za kuwepo katika benchi kutokana na mabadiliko ya kanuni za Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).
Alisema kuondolewa kwa makocha hao kumetokana na kukosa sifa kwa sababu Simba wangeshinda na kuingia makundi ni lazima wangeondoka kwa kubanwa na taratibu mpya.
“Kocha wa viungo na makipa hata kama tusingefungwa ilikuwa ni lazima waondoke tu maana kanuni haziwaruhusu kuwepo benchi na ndio maana kocha wetu msaidizi Suleiman Matola anasoma hivi sasa,” alisema.
Hata hivyo, chanzo kutoka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kilisema kuwa makocha hao wa Simba wanavyo vigezo vya kuwepo benchi kutokana na elimu zao kuwaruhusu na huenda wameachwa kwa mapenzi ya klabu.
“Kuwa kocha wa makipa unatakiwa kuwa na Level 2 ya ukocha wa makipa na kwa upande wa kocha wa viungo anatakiwa kuwa na walau Certificate ya Football Fitness kutoka CAF na FIFA ambazo makocha hao wa Simba wamekidhi,” alisema mtoa habari wetu kutoka ndani ya TFF ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Mwanaspoti ilimtafuta katibu wa Chama cha Makocha, Makka Malwisi ambaye alisema makocha wa Simba waliambiwa wawasilishe vyeti vyao, lakini suala la kocha kuachana na timu yake ni makubaliano ya pande mbili.
“Kama sifa za kukaa benchi wanazo basi kutakuwa na mambo mengine, lakini sisi tunatamani wazawa wenye elimu wapewe nafasi na ndio maana wageni wanabanwa kwa sasa,” alisema.
Beki wa zamani wa Coastal Union, George Mbwana ‘Bassanga’ alisema ni vyema Simba ikawapa nafasi makocha ambao walipita kutokana na uzoefu wao kuliko ambao hawaijui timu kabisa.
“Milovan ni kocha mzuri endapo akipata nafasi sawa, naamini alivyotoka mpaka atake kurudi anakuwa ameona upungufu na kuufanyia kazi,” alisema Bassanga.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: