YANGA VS AL HILAL MECHI YA KISASI


 

Leo , Jumanne ya Novemba 26, Yanga itaikaribisha Al Hilal kutoka Sudan katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo huu ni kama marudio ya ule wa Oktoba 2022, pale timu hizi zilipokutana kwenye raundi ya pili ya hatua ya awali kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Yanga ikitaka kurudi kwenye hatua ya makundi kwa mara ya kwanza ndani ya karne ya 21, ilitolewa kwa jumla ya mabao 2-1 kufuatia kufungwa 1-0 ugenini baada ya sare ya 1-1 nyumbani.

Mechi hiyo ni maarufu sana kwa kauli ya ‘Sudan Kugumu’ ya Rais wa Yanga, Mhandisi Hersi Said, aliyoitoa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere alipokuwa akirudi kutoka Sudan kwenye mechi ya mkondo wa pili.

Timu hizi mbili zinakutana huku zote zikiwa na sifa moja ya ‘UKIMBIZI’, kwa sababu tofauti.

AL HILAL
Jina lake likiwa na maana ya mwezi mchanga (Crescent), Al Hilal ni timu kubwa na yenye mafanikio kuliko zote nchini Sudan.

Inatokea jijini Khartoum katika wilaya ya Omdurman ambako inamiliki uwanja wake binafsi unaoitwa Al-Hilal Stadium au ukifahamika kwa jina la utani la The Blue Jewell yaani Lulu ya Bluu.

Uwanja huu wenye uwezo wa kubeba watazamaji zaidi ya 30,000, ulifunguliwa tangu mwaka 1968, mwaka ambao Yanga SC walihamia kwenye ofisi zao za kwanza za makutano ya mitaa ya Mafia na Swahili...kabla hata ya kupata kiwanja cha Jangwani ambacho sasa ndiyo makao yake makuu.

Al Hilal wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani, ni wanyama tofauti kabisa. Mashabiki wao wanajaa uwanjani na wanaishangilia timu yao kwa hisia kali sana.

Lakini machafuko ya kisiasa yameifanya timu hiyo sasa ikimbie nyumbani na kuishi ughaibuni.


Mwaka jana iliishi sana Dar es Salaam na kukaribia kukubaliwa kushiriki Ligi ya Kuu ya Tanzania Bara kama siyo mambo kubadilika baadaye.


Sasa hivi ilikuwa Libya, ambako pia pia iliishi kabla ya kuja Tanzania, wakati pia ikishiriki Ligi Kuu ya Mauritania ambako inaongoza katika msimamo. Maisha ya Al Hilal yamekuwa sawa na Wasudan wengine zaidi ya milioni mbili, wakiwemo wapinzani wao wakuu El Merreikh, ya ukimbizi.

Machafuko ya kisiasa ya nyumbani yameifanya timu hiyo kuwa wakimbizi kwa muda mrefu sana.


Wakati ikiwa hapa nchini, kocha wao Florent Ibenge alisema kuishi ugenini muda wote ni changamoto kubwa sana kwa wachezaji wake, ikizingatiwa hakuna hata mmoja kwenye timu yake ambaye hajaathiriwa na vita.

“Wachezaji wote raia wa Sudan, kila mmoja ameguswa na vita hivi. Mnaweza kuwa sehemu, ghafla inakuja taarifa kwamba mchezaji mmoja amefiwa na mjomba wake aliyeuawa kwenye machafuko...ni ngumu sana,” alisema Ibenge. 

YANGA
Jina lao la Kiswahili ni matokeo ya kutafuta urahisi wa jina lao rasmi la Kiingereza la Young Africans, ambalo maana yake ni Vijana wa Kiafrika.

Klabu hii ilianzishwa mwaka 1935 jijini Dar es Salaam katika kitongoji cha Kariakoo.


Baada ya kujitafuta kwa miaka mingi, hatimaye mwaka 1972 ilijipata ilipofanikiwa kupata uwanja katika eneo la Jangwani kwa msaada mkubwa wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amaan Karume, na Meya wa Jiji la Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Simba, Ramadhani Omar Kirundu.

Naam, Yanga walipata eneo walilonalo sasa kwa msaada mkubwa sana wa Ramadhani Omar Kirundu, aliyekuwa mwenyekiti wa Simba na Meya wa Dar es Salaam.

Lile eneo la Jangwani lilikuwa jalala kuu la Kariakoo kwa hiyo isingewezekana Yanga kulipata na kulifanya uwanja bila idhini ya Meya wa jiji.

Na kama angekuwa na roho mbaya au angeleta ushabiki wa Simba na Yanga, angeweza kuwabania, na historia ingekuwa tofauti leo hii.

Kwa hiyo baada ya kulipata eneo hilo, Yanga wakajenga jengo lao kubwa ambalo lipo hadi sasa, na wakajenga uwanja wa mazoezi na mechi waliouita Kaunda, ambao sasa ni historia.

Miaka ya 1970 hadi 1980 Yanga walicheza mechi zao kwenye Uwanja wa Kaunda, na miaka ya 2000 waliendelea kufanya mazoezi pale pamoja na kucheza mechi za kirafiki.

Lakini kwa miaka zaidi ya 10 sasa Yanga wamekuwa wakimbizi, baada ya kuhama kwao. Wanatangatanga, siyo kwa sababu za kisiasa kama wenzao Al Hilal, lakini ni kwa kukosa mipango na malengo kwa viongozi wao.

Japo mechi yao ya leo itachezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, lakini ni ya kwanza kwa klabu hiyo kongwe tangu wakimbie Uwanja wa Chamazi na kukimbilia Uwanja wa KMC pale Mwenge.

Al Hilal ni wakimbizi wa kulazimishwa, Yanga ni wakimbizi wa kujitakia.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.