MISA TAN YAHIMIZA WAANDISHI WA HABARI WANAWAKE KUTUMIA TEKNOLOJIA VIZURI KUPAMBANA NA TAARIFA POTOSHI KUKABILIANA NA UKATILI WA KIJINSIA MTANDAONI
Kauli hii imetolewa leo Jumatatu Novemba 25, 2024, na Mrajis wa Asasi za Kiraia nchini Zanzibar, Bw. Ahmed Khalid Abdulla, wakati akifungua mafunzo ya waandishi wa habari wanawake kuhusu usawa wa kijinsia katika vyombo vya habari.
Aidha amewataka wandishi hao kuepuka uandishi wenye vichwa vya habari vinavyo changanya jamii kwa lengo la kuuza magazeti au kutafuta wasomaji wengi kwenye mitandao huku kukiwa na upotashaji ndani ya habari hiyo.
Amesisitiza kuwa, waandishi hao wanapaswa kutumia majukumu yao vizuri kwa kutoa habari ambazo zitasaidia jamii kuelewa na kujenga nguvu za pamoja katika vita hii.
MISA TAN: Ushirikiano wa Waandishi wa Habari na Teknolojia
Mkurugenzi Mkaazi wa MISA TAN, Bi. Elizabeth Rizik, amesisitiza kuwa MISA TAN imekuwa ikishirikiana na waandishi wa habari katika kukuza ufanisi wao, ikiwemo kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa ili kuboresha upatikanaji na usambazaji wa taarifa muhimu kuhusu kupinga ukatili wa kijinsia.
Ameongeza kuwa, MISA TAN inaendelea kutumia fursa za teknolojia ili kuhakikisha taarifa zinazofikishwa kwa jamii zinahusiana na kulinda utu na kupinga ukatili wa kijinsia.
Uandishi wa Habari za Kidijitali: Changamoto na Fursa
Akiwasilisha mada kuhusu uandishi wa habari za kidijitali, Bw. Othman Maalim Othman ameonya kuhusu athari za matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Amesema kuna wimbi kubwa la vijana wanaotumia mitandao kurusha taarifa za kupotosha bila kuzingatia maadili ya uandishi.
Amewahimiza waandishi wa habari waliosomea kutumia nafasi zao kurekebisha taarifa potofu na kutoa habari zenye tija kwa jamii.
"Kwa sasa, kumekuwa na urahisi mkubwa wa kuifikishia jamii taarifa kupitia mitandao ya kijamii, lakini ni muhimu pia kuhakikisha kuwa taarifa hizi zina manufaa kwa jamii na kwa taifa kwa ujumla," amesema Bw. Othman.
"Wakati umefika kwa waandishi wa habari kutumia mitandao ya kijamii kwa kuzingatia maadili ya uandishi, ili kupunguza athari zinazojitokeza kutokana na taarifa za upotoshaji. Hii itafaidi taifa kwa kuhakikisha tunatumia teknolojia kwa maslahi ya maendeleo ya jamii."
Kupambana na Ukatili wa Kijinsia na Teknolojia za Kisasa
Mafunzo hayo ya waandishi wa habari wanawake yamejikita katika kuimarisha uandishi wa habari za kidijitali na matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kupambana na taarifa za upotoshaji na kuzuia athari za kijinsia zinazoweza kuzorotesha maendeleo ya jamii.
MISA TAN inatambua umuhimu wa waandishi wa habari katika kutoa taarifa zinazojenga na kuelimisha jamii kuhusu masuala muhimu, hususan kupinga ukatili wa kijinsia, kwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa njia inayozingatia maadili.
No comments: