Friday, January 24 2025

UTPC YAZINDUA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI MANYARA


MUUNGANO wa Klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC) umezindua kampeni maalum za siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto mwaka 2024 kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Kauli mbiu ikiwa 'Baada ya miaka 30 ya Beijing Tuungane kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana'.


Mkurugenzi mtendaji wa UTPC Kenneth Simbaya akizungumza kwenye uzinduzi huo uliofanyika Novemba 25 mjini Babati mkoani Manyara, amesema vyombo vya habari vina mchango mkubwa mno katika kutokomeza ukatili.

Simbaya amesema Waandishi wa Habari washirikishwe kuanzia mwanzo hadi mwisho kwenye mambo mbalimbali ili waweze kuandika kwa ufasaha taarifa tofauti kuliko kuwaita kwenye ufunguzi au uzinduzi wa jambo.


"Vyombo vya habari vinatawala akili za watu kwani haziwapangii jambo la kufikiri ila watu watafikiri kwa kina baada ya kupata taarifa kwenye vyombo vya habari," amesema Simbaya.

Amesema mchango wa vyombo vya habari katika kushiriki kufanikisha maendeleo ni mkubwa mno hivyo jamii na viongozi wa taasisi na Serikali wanapaswa kutoa ushirikiano kwao.


"Waandishi wa Habari wanapoandika mapungufu pia wanaangalia na mafanikio kwani Tanzania ya sasa siyo sawa na ya miaka iliyopita kwenye maendeleo," amesema Simbaya.

Mgeni rasmi wa uzinduzi huo Askofu Mkuu wa Kanisa la Elim Pentecoste Tanzania, Peter Konki amesema jamii ikipata elimu ipasavyo juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia itaachana nayo.


Konki amesema Manyara haipaswi kufurahia kuwa na matukio mengi ya unyanyasaji wa kijinsia hivyo ni muda wa kuachana na matukio hayo.


Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Manyara (MNRC) Zacharia Mtigandi amesema Mkoa wa Manyara ni Mkoa wa pili kati ya miaka 28 kwa ukatili wa kijinsia.

Mtigandi amesema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2021 Manyara ni ya pili Tanzania kwa visa 3,400 vya ukatili wa kijinsia ikitanguliwa na Iringa.

Amesema matukio mengi ya unyanyasaji wa kijinsia yanayotokea mkoani Manyara, ni ya vipigo,ubakaji na ukeketaji.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Manyara, Anna Fissoo amesema Manyara bila ukatili inawezekana hivyo jamii inapaswa kuongeza nguvu katika kupinga ukatili.

Fissoo amesema kila mmoja atimize wajibu wake katika kupinga ukatili kwani vitendo vya ukatili wa kijinsia bado vinafanyika mkoani Manyara.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.