WATU SITA WAKAMATWA WAKITOROSHA MADINI YA DHAHABU SHINYANGA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kukutwa wakitorosha madini ya dhahabu yenye uzito wa gramu 930.88 yenye thamani ya shilingi milioni 93.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Alhamisi Agosti 11,2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema tukio hilo limetokea Agosti 10,2022 majira ya tatu usiku katika barabara ya Ilogi kuelekea mkoa jirani wa Geita kata ya Bugarama halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga.
“Askari Polisi wakiwa katika doria walilitilia mashaka gari lenye namba za usajili T 913 DRX Toyota Land Cruiser rangi ya njano na kulisimamisha ndani ya gari hilo hilo kulikuwa na watu sita na upekuzi ulipofanyika kwa kushirikiana na Idara zingine za serikali ambapo tulifanikiwa kukuta madini ya dhahabu yenye uzito wa gramu 930.88 yenye thamani ya shilingi 93,000,000/= na pesa taslimu 97,025,000/=”,amesema Kamanda Magomi.
Ameeleza kuwa pia walikuta mzani mmoja wa kielektroniki wa kupimia dhahabu pamoja na mashine moja ya kupima ubora wa dhahabu.
Kamanda Magomi amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa watuhumiwa walikuwa wakitorosha madini hayo ya dhahabu kwenda nje ya nchi kwa lengo la kukwepa kodi na tozo za serikali kitendo ambacho ni kosa kisheria.
“Taratibu za kipolisi kama wasimamizi wa sheria zitakapokamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani. Nitoe rai kwa wananchi wanaojihusisha na shughuli za kutafuta kipato kupitia biashara ya madini wafuate sheria zilizopo ili kuinua kipato cha familia na pato la taifa kwa ujumla”,amesema.
Chanzo - Malunde blog
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: