TGNP, AGA KHAN WATOA MAFUNZO KWA WARAGHBISHI NGAZI YA JAMII UTEKELEZAJI WA MRADI WA TUINUKE PAMOJA
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Lilian Liundi akifungua mafunzo ya Uraghbishi kwa Waraghbishi kutoka ngazi ya jimii katika wilaya za Chemba, Kondoa TC, Kondoa DC, Mkoani Dodoma
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Aga Khan Foundation kupitia Mradi wa Tuinuke Pamoja unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania wametoa mafunzo ya Uraghbishi kwa Waraghbishi kutoka wilaya za Chemba, Kondoa TC na Kondoa DC, mkoani Dodoma.
Mafunzo hayo yanafanyika kuanzia tarehe 04 hadi 07 Februari, 2025, Jijini Dar es Salaam na lengo kuu ni kuimarisha uwezo na ujuzi wa Waraghbishi katika kuongoza na kuwezesha ujenzi wa usawa wa kijinsia na ukombozi wa wanawake kwa kutumia mbinu za Shirikishi katika ngazi ya jamii.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, amesema malengo ya mafunzo hayo ni kujenga uelewa wa dhana za jinsia na itikadi ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi.
"Lengo ni kukuza uelewa wa falsafa ya Uraghbishi kwa kutumia mbinu ya “U” tatu (Upimaji, Uchambuzi, na Utekelezaji) kwa vitendo, pamoja na kuibua na kuchambua masuala ya kijinsia kwa kutumia mbinu na nyenzo mbalimbali za kiraghbishi. Vilevile, mafunzo haya yatasaidi kuimarisha ujuzi wa uchambuzi na shirikishi (PAR) pamoja na utunzaji wa kumbukumbu na uwezo wa kuutumia katika utekelezaji wa miradi ngazi ya jamii",ameeleza Liundi.
Lilian Liundi amesema kwa mara ya kwanza, mradi huu umeonyesha utofauti mkubwa kwa kuzingatia kwamba ruzuku itatolewa moja kwa moja kwa vikundi vya jamii, jambo ambalo linarahisisha utekelezaji wa miradi na kujenga uwezo wa haraka kwa vikundi vya wanawake.
Amesisitiza kuwa, ingawa mashirika makubwa ya kitaifa mara nyingi hupokea ruzuku kutoka kwa wafadhili, mradi huu umeleta mabadiliko kwa kuwatengenezea fursa wanawake, ambao ndiyo wanaoathirika zaidi na masuala ya umaskini na ukatili wa kijinsia.
Ameeleza kuwa, Mradi huu wa Tuinuke Pamoja unalenga kuwawezesha wanawake wengi, ambao mara nyingi wamekuwa wakiathirika zaidi na changamoto za kijinsia, ukatili, na umaskini.
"Lengo kuu ni kuboresha nafasi ya wanawake katika nyanja za uongozi na kumiliki uchumi, kwani hadi sasa, idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi na kumiliki mali bado ni ndogo",amesema.
Lilian ameelezea kuwa mradi huu ni muhimu kwa sababu unatoa fursa kwa wanawake wengi katika jamii ya vijijini, ambapo masuala ya kijinsia yanaonekana kutokuwa na usawa, na mara nyingi wanawake hawa wanakutana na changamoto kubwa.
Mradi huu ni chachu ya mabadiliko katika kuboresha maisha ya wanawake, kuimarisha uongozi wao na kuongeza usawa wa kijinsia katika jamii.
Mafunzo haya ya Uraghbishi yana nafasi muhimu katika kuhamasisha na kuimarisha juhudi za kijinsia, na pia kutoa ujuzi wa kuchambua masuala ya kijinsia na kutatua changamoto zinazowakumba wanawake na utaendelea kutoa matokeo chanya na kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii.
Meneja Mradi Tuinuke Pamoja Nestory Mhando akizungumza namna mradi utakavyofanya kazi katika wilaya za Chemba, Kondoa TC, Kondoa DC mkoani Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Uraghbishi kwa Waraghbishi kutoka ngazi ya jimii yanayofanyika katika ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) jijini Dar es Salaam.
Baadhi wa Waraghbishi na wafanyakazi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wakifuatilia hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Lilian Liundi alipokuwa anafungua mafunzo ya siku nne ya Waraghbishi kutoka ngazi ya jimii katika wilaya za Mkoa wa Dodoma
Picha ya pamoja.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: