YANGA YAITENGEA SIMBA SIKU 10 NZITO ZA MAANGAMIZI
IMEBAKI kama mwezi mmoja kabla ya watani wa jadi nchini, Simba na Yanga kuvaana kwenye mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Desemba 11.
Hata hivyo, wakati mechi hiyo ikiwa jirani, Yanga inaonekana kuizidi ujanja Simba katika maeneo mawili ambayo pengine watani wao wasingependa iwe hivyo kabla ya mchezo huo utakaokuwa wa 107 kwa timu hizo kukutana ndani ya Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965.
Eneo la kwanza ni kutanguliwa kwao kwa tofauti na pointi nne baada ya michezo mitano ya kwanza, hivyo kama timu hizo mbili zitapata ushindi katika michezo ya ligi iliyobakia kabla ya kukutana maana yake Yanga itaingia uwanjani Desemba 11 ikiwa haina presha kubwa kwani matokeo yoyote itakayopata yataifanya iendelee kubakia kileleni.
Lakini ukiweka kando hilo, Yanga itaingia katika mechi hiyo ikiwa imepata muda mrefu na wa kutosha kujiandaa nao kulinganisha na Simba wanaokabiliwa na ratiba ngumu kutokana na ushiriki wake katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga itapata muda wa takriban siku 10 kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya Simba kwani itacheza mechi yake ya mwisho kabla ya kuwavaa watani zao, dhidi ya Mbeya Kwanza, Novemba 30.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Yanga, Simba yenyewe itakuwa na siku tano tu za maandalizi zinazoweza kupungua zaidi ikiwa watakumbana na changamoto ya usafiri kwani wenyewe watacheza mchezo wao wa mwisho kabla ya kuivaa Yanga Desemba 5 ugenini huko Zambia utakaokuwa ni wa marudiano wa hatua ya mwisho ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: