HABARI MPYA LEO KUTOKA SIMBA SC, OKWI, CHAMA NA MIQUISSONE WATAJWA
LICHA ya Ligi Kuu Bara kuwa na timu nyingi, lakini Simba ni inawauza nyota wake bila kujali umuhimu ndani ya kikosi.
Simba imekuwa tofauti na timu zingine mchezaji akipata ofa ya timu nyingine hasa nje ya nchi, basi huwauza pasipo kujali ni namna gani itawagharimu baadaye.
Hawa hapa ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa kikosi cha kwanza, lakini walipopata ofa uongozi uliwauza bila kujali.
LUIS MIQUISSONE
Kiwango bora alikionyesha msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Luis ni mmoja wa wachezaji waliokuwa na uhakika na namba ndani ya kikosi hicho, lakini baada ya Al Ahly ya Misri ambayo Simba walikutana nayo katika michuano hiyo kutuma ofa, haikupingwa.
Kuondoka kwa Luis aliyekuwa msaada mkubwa wa mashambulizi pengo lake linaonekana ndani ya kikosi hicho kinapocheza.
SHIZA KICHUYA
Nyota huyu aliondoka Simba ikiwa katika kiwango cha hali ya juu na kwenda kujaribu maisha mapya Pharco FC ya Misri.
Wakati huo Simba ilikuwa inanolewa na Joseph Omog, lakini Shiza alikuwa mwiba wa kupiga kona hadi kusababisha kubatizwa jina la ‘Kona Goli ndani ya kikosi hicho.
EMMANUEL OKWI
Huyu ni kipenzi cha wana Simba miaka yote. Ni mmoja wa wachezaji waliokuwa na mchango mkubwa kikosini.
Lakini, baada ya Etoile du Sahel ya Tunisia kuwasilisha ofa kumhitaji nyota huyo, Simba hawakuona shida, bali walimruhusu kwenda kujaribu maisha kwingine licha ya baadaye kurudi na kuondoka tena.
Mambo makubwa Okwi aliyoyafanya ndiyo tiketi iliyomfanya wana Msimbazi kumwamini na kumpenda, huku ikidaiwa huenda akarejea tena.
CLATOUS CHAMA
Alibatizwa jina la Mwamba wa Lusaka. Ni kiungo fundi aliyejipatia tuzo ya kiungo bora wa msimu, lakini baada ya RS Berkane ya Morocco kupeleka ofa Simba hakukuwa na hiyana, bali walimuachia akajaribu maisha mengine.
Chama aliondoka Simba baada ya msimu uliopita kumalizika, lakini umuhimu wake unaonekana wazi kuanzia mchezo wa Ngao ya Jamii, Ligi Kuu pamoja na wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy na kuwafanya wana Simba wamkumbuke.
MAWETE MUSOLO/MWANAHAMIS OMARY
Mbali na timu ya wanaume, hata ya wanawake ‘Simba Queens’ imekuwa haijali mchezaji husika - kwa maana ya kuwakumbatia ili waileteee mafanikio zaidi, lakini ikitokea ofa hukaa na kukubaliana na kuwaachia.
Msimu uliopita pengo la Mwanahamis lilionekana baada ya kupata shavu Morocco katika klabu ya Shabab Atlas. Zipo taarifa pia za Mawete Musolo kuondoka Simba Queens ikidaiwa katimkia Uturuki huku pia Oppa Clement inasemekana yupo mbioni kuuzwa Morocco.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: