UKWELI KUHUSU MAUZAUZA YALIYOPO KIJIJI CHA KICHAWI GAMBOSHI KILICHOPO MKOANI SIMIYU

GAMBOSHI ni kijiji kinachopatikana Kata ya Gamboshi wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu. Ni takribani kilometa 37 kutoka makao makuu ya Mkoa wa Simiyu mjini Bariadi.

Gamboshi siyo jina geni sana kwako unayesoma makala simulizi, lakini nitajitahidi mno kuhakikisha nakuletea ukweli kuhusu Gamboshi.

Gamboshi kinatambulika kama kijiji ambacho ndiko makao makuu ya wachawi nchini Tanzania, yaani ni maarufu kwa jina la Ikulu ya Wachawi Tanzania! Kinaelezwa kuwa ni kijiji chenye maajabu makubwa.

Historia ya kijiji hiki imesambaa ndani na nje ya Tanzania. Kumekuwa na simulizi nyingi mno za kutisha. Hii ndiyo sababu inayoweza kufanya kuwa Gamboshi lisiwe jina geni kwako.

Kwa bahati mbaya au nzuri, simulizi hizi zimekuwa siyo nzuri hata kidogo.

Kijiji hiki kinatambulika kwa kila Mtanzania kuzidi hata jina la wilaya au mkoa. Waandishi wa habari mbalimbali hapa nchini baadhi yao wamefanikiwa kufika katika kijiji hiki na wengine kukwamia njiani.

Waliofanikiwa kufika ndiyo wamesababisha Gamboshi kujulikana kwa kiwango hicho, lakini pia baadhi ya wananchi ambao baadhi yao ni wazawa wamekuwa wakitoa simulizi za kijiji hicho kupitia vyombo vya habari.

Simulizi na habari hizo zinaeleza kuwa, kijiji hicho kimejaa mauzauza (miujiza). Inaelezwa kuwa, ikifika usiku, Gamboshi hubadilika, inaonekana kama mmoja wa mji mkubwa (Cairo), nyumba nyingi zenye ghorofa zaidi ya 50.

Mchana kijiji hiki kinaonekana kawaida, mandhari yake ya kawaida kabisa ya kijijini; nyumba za nyasi na fupi, lakini usiku kunabadilika. Kijiji kinaonekana kama jiji, taa za wakawaka, jiji linalong’aa.

Kutokana na historia ya Gambosi kuwa ya kutisha na ambayo imesambaa nchi nzima, kuna madai kuwa, tangu Tanzania ipate uhuru hakuna kiongozi yeyote wa dini au serikali mkuu ambaye amefika, taarifa ambazo si za kweli.

Julai 27, 2016 ni siku ambayo wananchi wa kijiji hicho walipata furaha ambayo inayotajwa kuwa haijawahi kuonekana. Ni siku ambayo Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu alikanyaga ardhi ya Gamboshi.

Askofu Sangu alifika kijijini hapo kwa ajili ya kuzindua Kanisa Katoliki Kigango cha Gamboshi.
Inaelezwa kuwa kanisa hilo limejengwa kwa nguvu za wananchi wa kijiji hicho, hali inayoshangaza kidogo.

Ilikuwa furaha kubwa kwa wananchi wa Gamboshi mara baada ya kuwasili kwa kiongozi huyo, wenyewe walisema haijawahi kutokea kiongozi mkubwa wa serikali hata wa dini kufika kijijini hapo.

Historia mbaya imekuwa ikiwaandama wanakijiji na kuwafanya kuonekana watu ambao ni hatari. Umati wa wanakijiji hicho pamoja na wanafunzi, unafurika kanisani hapo kwa ajili ya kumuona Askofu Sangu, huku wengine wakitamani kumshika hata mkono au nguo zake.

Wakati mwingine Askofu Sangu alijikuta amezungukwa na umati, huku wasaidizi wake wakishindwa kuwazuia kutokana na furaha waliyonayo akiwa na askofu mwenyewe.

Haikuwahi kutokea hata siku moja kabla ya hapo. Historia iliwafanya wanakijiji wa Gamboshi kujiona wanyonge kila sehemu, unapotoka nje ya Gamboshi ukaelekea sehemu nyingine wakati mwingine unalazimika usitaje unapotoka.

Wananchi hao walieleza kuwa ujio wa kiongozi huyo ni neema kubwa kwao na unakuwa mwanzo wa kuweza kubadilisha mawazo hasi ya Watanzania na nje ya nchi juu ya kijiji chao ambayo yamedumu vichwani mwao.

Wanakijiji hao wanashikilia msimamo wao kuwa siyo kweli kwamba Gamboshi ni makao makuu ya wachawi, badala yake wanaeleza hapo zamani kulikuwa na familia mbili ambazo zilikuwa zikishindana kwa uchawi.

Wanaeleza familia hizo ni Mwanamabula na Mwanamakulyu, ambao walikuwa wakishindana kwa uchawi, hali ambayo ilikuwa ikiwavutia watu mbalimbali hapa nchini kufika kijijini hapo kwa ajili ya kuchukua dawa.

Waliokuwa wakichukua dawa ndiyo waliopeleka habari hizi mbaya kwa Watanzania wengine tangu zamani hiyo mpaka leo historia haijafutika.

Itaendelea wiki ijayo.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.