WALIMU WAMFUNGIA MKUU WA SHULE NDANI YA OFISI

Walimu wa Shule ya Sekondari Bondeni iliyopo jijini Arusha, wamemfungia ndani ya ofisi mkuu wa shule hiyo, Rahim Massawe kwa kushindwa kushughulikia malimbikizo ya mishahara yao inayofikia kiasi cha Sh 10 milioni kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo.

Wakizungumza leo Ijumaa na waandishi wa habari ofisini hapo, walimu hao wamesema kuwa wamefikia hatua ya kufanya hivyo kama sehemu ya kushinikiza madai yao ya kulipwa malimbikizo ya mishahara yao ambayo wamekuwa wakiidai kwa kipindi kirefu bila mafanikio.

Mwalimu Rose Sechume amesema kuwa shule hiyo hapo awali wakati ikiendeshwa na Bakwata mkoani hapa walikuwa wakilipwa mishahara yao bila shida yoyote ila tangu wameingia ubia na mwekezaji wa kampuni ya Zaim Education Development ambayo ilikabidhiwa shule hiyo tangu Septemba mwaka huu mambo mengi yamekuwa hayaendi likiwemo suala la malipo yao.

Kwa upande wake mwalimu Shaban Hungo amesema tangu kukabidhiwa shule hiyo mikononi mwa kampuni hiyo kumekuwa na mapungufu mbalimbali ikiwemo kukusanya ada za wanafunzi na kushindwa kulipa wafanyakazi, kufukuzwa shule kwa wanafunzi wasiomaliza ada na kunyimwa kufanya mitihani, pamoja na kuongeza ada mara mbili zaidi, kutoka wastani wa Sh 600,000 mpaka Sh 1.2 milioni.

Hungo amesema kuanzia Shule hiyo ikabidhiwe mikononi mwa kampuni hiyo imechangia kiwango cha elimu kushuka huku wanafunzi wakipoteza motisha wa kusoma kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu kwa kipindi hicho cha miezi mitatu mfululizo.

"Tumejaribu kukaa na mwalimu mkuu ili tuzungumze kila wakati anatupa majibu yasiyoeleweka sasa tumeamua kumfungia ndani mpaka huyo mwajiri wake atakapofika hapa na kutupa jibu juu ya hatima ya malipo yetu," amesema mwalimu Hungo.

Mkuu wa shule hiyo, Rahim Massawe aliyefungiwa ndani ya ofisi akizungumzia suala hilo kupitia dirisha la ofisi hiyo amesema yeye binafsi aliwaita walimu hao ofisini kwake kuzungumzia suala hilo lakini ameshangaa wanashindwa kufikia muafaka na kuamua kumfungia ndani ya ofisi.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.