KAMATI YA BUNGE YAKERWA NA KITENDO CHA POLISI KUWAINGILIA KWA KUWAKAMATA WAANDISHI

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imelaani kitendo cha jeshi la polisi kumkamata na kumhoji mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe, Agusta Njoji kutokana na habari aliyoiandika mwishoni mwa wiki.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Nagenjwa Kaboyoka aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kitendo kilichofanywa na polisi Mkoa wa Dodoma ni kutaka kuminya na kuficha maovu ambayo yamejaa ndani ya jeshi hilo.

Njoji aliandika habari kutoka kwenye kamati hiyo wakati PAC ilipokutana na viongozi wa polisi kwa lengo la kutaka ufafanuzi kuhusu manunuzi ya magari ya polisi maarufu washawasha pamoja na mchakato wake wakihoji kutokana na taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).

Kufuatia taarifa hiyo, Polisi Mkoa wa Dodoma walimuita na kumhoji na kisha kuamuru awekwe ndani kabla ya Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi Dodoma (CPC), Habel Chidawali kumwekea dhamana kwa bondi ya Sh 5 milioni.

Nagenjwa alikiri kuwa taarifa zilizoandikwa na magazeti ya Nipashe na Mwananchi mwishoni mwa wiki zilikuwa sahihi lakini akashangazwa kwa polisi kuamua kuwasumbua waandishi wa habari.

“Nisema kuwa, kazi zetu kwa sehemu kubwa zinawategemea waandishi wa habari, tumesikitishwa sana na tumeamua kumwandikia barua Spika wa Bunge kutaka ufafanuzi ili kuondoa mkanganyiko wa utendaji wa kazi zetu kuliko kuingiliwa mara kwa mara na wengine,” alisema Kagoyoka

Kwa mujibu wa maelezo ya Kaboyoka, kabla ya kumuandikia spika barua ya kutaka maelezo ya utendaji kazi wa kamati, walimtuma ofisa wa bunge kwenda kuzungumza na polisi ili kujua ukweli wa mambo ulivyo na kwamba polisi walikiri kukosea na wakaahidi kulifuta jalada hilo.

Wakati kamati ikiwaita waandishi kuzungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa CPC, Habel Chidawali na katibu wake Bilson Vedastus waliitwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Mroto kwa ajili ya kuzungumzia sakata hilo.

Kwa mujibu wa Chidawali, Mroto aliwataka waandishi kuendelea na majukumu yao kwani wito kwake kwa mwandishi huyo ulilenga kujua ukweli wa chanzo cha habari hiyo na hivyo akasema kuwa yamekwisha.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.