
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga, amesema Jeshi la Polisi mkoani humo, linamshikilia Mashaka Mwoga (36), mkazi wa Chipaka mjini Tunduma wilayani Momba, kwa tuhuma za kumuua mke wake, Bi. Gloria Anton (32) kwa kumnyonga sababu ya wivu wa mapenzi.
Kamanda Senga amesema baada ya kupokea taarifa hiyo, polisi na ndugu wa marehemu walimtilia mashaka mtuhumiwa na kumkamata hadi alipokiri kuhusika na mauaji kisha kwenda kuonesha sehemu alikoutupa mwili wa mkewe.
Kamanda Senga ameeleza kuwa walimbaini mtuhumiwa kuwa alimnyonga mke wake tangu Machi 8, 2025 na kuazima gari la rafiki yake na kubeba mwili kwenda kuutupa katika shamba la mahindi lililopo Kijiji cha Chiwanda, Kata ya Nkangamo umbali wa meta 50 kutoka barabara kuu ya Tunduma kwenda Sumbawanga.
Mtuhumiwa baada ya kuhojiwa alikiri kutenda mauaji hayo na kuonesha mahali alipoutupa mwili wa marehemu na Machi 13, 2025, polisi waliupata mwili huo ukiwa tayari umeharibika.