
Mwanamke aitwaye Agatha Daniel Nyahuma (32), mkazi wa Bugayambelele, kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga, amefariki dunia baada ya kukatwa kwa kitu chenye ncha kali mgongoni na mtu au watu wasiojulikana.
Inaelezwa kuwa tukio hili limetokea Jumapili, Machi 9, 2025, majira ya saa 12:30 asubuhi, katika mtaa wa SIDO uliopo Buhangija kata ya Ibinzamata, Manispaa ya Shinyanga ambapo Agatha alikuwa akielekea katika Kanisa Katoliki Parokia ya Buhangija kutoka nyumbani kwake.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Kenedy Mgani amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo akisema mpaka sasa Jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo ili kujua chanzo na wahusika.
"Agatha alikuwa anatoka nyumbani kwenda kanisani akiwa njiani ghafla alijeruhiwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya mgongoni chini ya bega la mkono wa kulia na mtu/watu wasiofahamika, alianguka kutokana na hilo jeraha,akachukuliwa na wasamaria wema akakimbizwa hospitali ya Manispa ya Shinyanga lakini wakati anaendelea kupata matibabu alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi",amesema Mgani.