Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam, Tanzania – Jumamosi, 1 Agosti 2026: Uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China umedhihirishwa tena kupitia Mashindano ya 13 ya Mpira wa Kikapu ya Jamii ya Wachina yaliyofanyika katika Viwanja vya Don Bosco, Namanga.
Mashindano hayo yamefunguliwa rasmi na Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa, na kudhaminiwa na Stanbic Bank kwa Shilingi milioni 30. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Msigwa alisema michezo inaendelea kuwa chombo muhimu cha kuimarisha mahusiano kati ya wananchi wa nchi hizo mbili.
"Uhusiano kati ya China na Tanzania una historia ndefu na unaendelea kuimarika kupitia matukio kama haya ambapo michezo inatuunganisha katika roho ya urafiki na kuheshimiana. Naipongeza Stanbic Bank kwa kuendelea kudhamini mashindano haya kwa miaka mingi," alisema.
Mbali na kuwa mdhamini mkuu, Stanbic Bank pia imeshiriki mashindanoni kupitia timu yake ya mpira wa kikapu. Ushiriki huo unaonyesha namna benki hiyo ilivyojitoa kikamilifu katika kuunga mkono jamii ya Wachina nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji (Corporate and Investment Banking) wa Stanbic Bank Tanzania, Ester Manase, alisema udhamini huo ni sehemu ya dhamira ya benki ya kujenga ushirikiano unaovuka huduma za kifedha.
"Kwa miaka mingi, mashindano haya yamekuwa moja ya majukwaa muhimu kwetu katika kuimarisha mahusiano na jamii ya Wachina nchini Tanzania kwa sababu tunaamini ushirikiano imara hujengwa kupitia uzoefu wa pamoja, si miamala ya kifedha pekee. Dhamira hiyo ndiyo msingi wa kazi yetu kupitia Standard Bank Group, ushirikiano wetu na ICBC pamoja na dawati letu maalum la huduma kwa wafanyabiashara wa Kichina," alisema Manase.
Aliongeza kuwa:"Udhamini wetu wa Shilingi milioni 30 una maana kubwa zaidi ya kugharamia mashindano. Kwa kushiriki kama mdhamini na pia mshindani, tunaonyesha kuwa ushirikiano wetu ni wa dhati na wa muda mrefu. Tunaendelea kuunga mkono mipango inayokuza mshikamano wa jamii, kubadilishana tamaduni na maendeleo ya pamoja."
Mashindano hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuleta pamoja wafanyabiashara wa Kichina, viongozi wa jamii na wadau mbalimbali katika mazingira ya urafiki na ushirikiano kupitia michezo.
Kadri ushirikiano huo unavyoendelea kukua, Stanbic Bank itaendelea kuimarisha uhusiano wake na jamii ya Wachina nchini Tanzania pamoja na kuunga mkono majukwaa yanayochochea ushirikiano, maelewano na maendeleo ya pamoja.











0 Comments