
📌 Atembelea Banda la Maliasili na Utalii Maonesho ya Nane Nane
📌 Asema rasilimali za utalii zinaangaliwa na wengi hivyo ni budi kuenziwa
📌 Aipongeza Wizara kwa kazi nzuri ya kutangaza utalii na vivutio vyake nje ya nchi
Na Neema Chalila Mbuja, Dodoma
NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Milya leo Agosti 02, 2026, ametembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye Maonesho ya Siku ya Wakulima Duniani ( Nane Nane) yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.
Baada ya kuwasili kwenye Banda la Wizara ya Maliasi na Utalii, Naibu Waziri Milya alipata fursa ya kuzungumza na wadau mbalimbali wa Sekta ya Utalii sambamba na kujionea uwepo wa wanyamapori hai kwenye maonesho hayo kama kivutio ili kukuza utalii wa ndani.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuitangaza Sekta ya Utalii nje ya mipaka ya Tanzania na kumpongeza kwa kuwa kinara kwenye sekta hiyo.
“Niwapongeze sana Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi kubwa mnayoifanya kwenye Sekta ya Utalii, Wanyamapori, Misitu na Nyuki na Malikale kwani kazi hii inalenga kutunza rasilimali tulizonazo Kama nchi,” amesema Mhe. Milya.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Nigeria aliyeambatana na Naibu Waziri Milya, Mhe. Hannafi Luqman amesema Tanzania na Nigeria zimekuwa na ushirikiano mzuri wa kidiplomasia na kuongeza kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele kutunza na kutangaza rasilimali ilizonazo.
Awali kabla ya kupokea ugeni wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Maliasili na Utalii ilipokea ujumbe wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena pamoja na Naibu Katibu Mkuu wake Dkt. Fabian Madele ambapo kwa pamoja walipata fursa ya kutembelea banda la Wizara na kuzungumza na wadau mbalimbali wa uhifadhi na wanyamamapori.
Wizara ya Maliasili na Utalii kwa pamoja na taasisi zake 18 inashiriki Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane yanayoendelea Viwanja vya John Malecela Nzuguni Dodoma ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba aliyafungua rasmi hapo jana.
0 Comments