BANGI YASHUKA KWA ASILIMIA 56, KRATOM YABAINIKA TANZANIA

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imeeleza kuwa juhudi za kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini zimeendelea kuzaa matunda, huku tani 1,017.26 za bangi zikikamatwa mwaka 2025 pamoja na tani 29.52 za dawa mpya aina ya Kratom zilizonaswa kwa mara ya kwanza nchini.

Taarifa hiyo iliwasilishwa leo Mei 29, 2026 bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, wakati akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa mwaka 2025.

Profesa Kabudi alisema uwasilishaji wa taarifa hiyo ni utekelezaji wa Kifungu cha 66 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015 kinachoielekeza Serikali kuwasilisha taarifa hiyo bungeni kila mwaka kwa lengo la kuonesha uwajibikaji na kutathmini utekelezaji wa mikakati ya mapambano dhidi ya dawa hizo.


Alisema pamoja na bangi kuendelea kuwa dawa ya kulevya iliyokamatwa kwa kiwango kikubwa zaidi, kiasi hicho kimepungua kwa asilimia 55.97 ikilinganishwa na mwaka 2024 kutokana na operesheni za uteketezaji wa mashamba makubwa ya bangi na kuimarika kwa hatua za udhibiti pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, tani 26.36 za mirungi pia zilikamatwa mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 42.88 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

"Takwimu hizi zinaashiria kuimarika kwa operesheni za ufuatiliaji na udhibiti hususan katika maeneo ya mipaka na njia zinazotumika kusafirisha dawa hizo," alisema.

Katika kundi la dawa za kulevya za viwandani, Serikali ilikamata kilogramu 907.18 za methamphetamine, kilogramu 672.23 za heroin, kilogramu 4.89 za cocaine, gramu 178 za MDMA pamoja na gramu 7.82 za MDA.

Profesa Kabudi alisema mwaka 2025 pia ulishuhudia kukamatwa kwa mara ya kwanza kwa tani 29.52 za Kratom, dawa inayotokana na mmea wa Mitragyna speciosa, ambayo iliingizwa nchini ikiwa imeelezwa kuwa ni mbolea kabla ya uchunguzi kubaini kuwa ni dawa ya kulevya.

Mbali na dawa hizo, Serikali ilikamata tani 31.76 na lita 183.5 za kemikali bashirifu pamoja na kilogramu 2.36 na mililita 160 za dawa tiba zenye asili ya kulevya kupitia ukaguzi uliofanyika katika vituo vya forodha, vyombo vya usafiri, kampuni za usafirishaji wa vifurushi na biashara za kemikali.

Kwa upande wa sheria, Waziri huyo alisema mashauri 1,124 ya dawa za kulevya yalifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini mwaka 2025. Aidha, mashauri 1,373 yalitolewa hukumu na Jamhuri ilifanikiwa kushinda mashauri 1,058.

Aliongeza kuwa mali zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.3 zilizohusishwa na makosa ya dawa za kulevya zilitaifishwa.

Katika sekta ya afya, jumla ya watu 85,425 wenye uraibu wa dawa za kulevya walipata huduma za tiba na utengamao kupitia vitengo vya afya ya akili, kliniki za MAT na nyumba za upataji nafuu zilizopo nchini.


Profesa Kabudi alisema mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na ushirikiano kati ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, vyombo vya ulinzi na usalama, wataalamu wa afya, wadau mbalimbali na wananchi.

Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo husika kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria vya biashara na matumizi ya dawa za kulevya ili kuimarisha usalama wa taifa na kulinda afya ya jamii.

Post a Comment

0 Comments