
Mtwara, 21 Mei 2026.
Raia wa Iran, Jan Mohammed Millan, aliyekuwa nahodha wa jahazi la Al Arab, amehukumiwa kifungo cha jumla ya miaka 60 jela baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha kilogramu 504.36 za heroin na kilogramu 355 za methamphetamine katika Bahari ya Hindi ndani ya eneo la kiuchumi la Tanzania.
Hukumu hiyo ilitolewa leo na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Sylvester Kainda, katika Kesi Na. 12657/2025 baada ya mshtakiwa huyo kukiri mashtaka yote mawili yaliyokuwa yanamkabili chini ya Kifungu cha 16(1) na 16(2)(c) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 Marejeo ya mwaka 2023.
Mahakama ilielezwa kuwa Aprili 22, 2021, Jan Mohammed Millan alikuwa akiiongoza jahazi la Al Arab akiwa na mabaharia wengine sita raia wa kigeni wakati wakisafiri katika Bahari ya Hindi karibu na pwani ya Kilwa mkoani Lindi, ndani ya Exclusive Economic Zone ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa upande wa Jamhuri, operesheni maalumu iliyohusisha maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha Majini, Jeshi la Polisi pamoja na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), ilifanikiwa kulinasua jahazi hilo baharini kabla ya kufanya upekuzi uliobaini uwepo wa shehena kubwa ya dawa za kulevya.
Mahakama ilielezwa kuwa katika upekuzi huo, maofisa walikamata heroin yenye uzito wa kilogramu 504.36 pamoja na methamphetamine kilogramu 355 zilizokuwa zimefichwa ndani ya jahazi hilo lililokuwa likitokea nje ya nchi.
Upande wa Jamhuri uliwasilisha vielelezo saba mahakamani, ikiwamo nyaraka za ukamataji, taarifa za upekuzi, exhibits, seal numbers pamoja na ripoti ya uchunguzi kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali iliyothibitisha kuwa dawa hizo ni heroin na methamphetamine.
Akitoa hukumu iliyochukua zaidi ya saa tatu, Jaji Kainda alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi uliowasilishwa pamoja na kukiri kwa mshtakiwa mwenyewe, huku ikibaini kuwa kosa hilo lina athari kubwa kwa afya ya jamii, usalama wa taifa pamoja na uchumi wa nchi.
“Tanzania haiwezi kuruhusu mipaka yake ya bahari kutumika kama njia ya biashara haramu ya dawa za kulevya zinazohatarisha maisha ya wananchi,” alisema Jaji Kainda.
Mahakama ilimhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka 30 kwa kila shtaka, hivyo jumla ya miaka 60 jela.
Katika hatua nyingine, washtakiwa sita waliokuwa mabaharia ndani ya jahazi hilo waliachiwa huru baada ya upande wa Jamhuri kueleza kutokuwa na nia ya kuendelea nao chini ya Kifungu cha 50 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Aidha, mahakama ilieleza kuwa methamphetamine yenye uzito wa kilogramu 355 tayari ilishateketezwa kwa moto, huku heroin kilogramu 504.36 ikipewa amri ya kuteketezwa kwa mujibu wa sheria. Jahazi la Al Arab nalo limetaifishwa na kuwa mali ya Serikali.
Mshtakiwa amepewa haki ya kukata rufaa ndani ya siku 30 endapo hataridhishwa na hukumu hiyo.
Hukumu hiyo inaendelea kuonyesha msimamo mkali wa mahakama na vyombo vya dola katika vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya na makosa ya uhujumu uchumi nchini.













0 Comments