DKT. SAJAD HABIB RAI AISHAURI SERIKALI KUANZISHA MFUKO WA MAFUTA

   

SERIKALI imeshauriwa kuanzisha Mfuko maalumu wa kuhimili bei ya Nishati ya mafuta nchini ambao pamoja na mambo mengine utasaidia kupunguza makali ya bei wakati wa dharura zinazosababishwa na sababu mbalimbali.

Rai hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na mdau wa Sekta ya mafuta nchini na Meneja mkazi  wa 'Mansoor Industries Ltd' Dkt Sajad Habib Rai alipozungumzia mwenendo wa upatikanaji Nishati hiyo.

Akizungumza kuhusu mfuko huo utakaotoa ruzuku, Dkt Sajad amesema kimsingi uwepo wake siyo utapunguza makali ya bei kwa wasafirishaji na wananchi peke yake bali pia kutasaidia kulinda uchumi wa nchi na hivyo kuliwezesha Taifa kupiga hatua.

Amesema kama ilivyo katika sekta zingine, uwepo wa mifuko katika sekta ya Nishati ya mafuta, kitarahisisha suala zima la upatikanaji wake hasa kwa waagizaji wakubwa wa mafuta hayo ambao wataweza kuagizia nishati hiyo kwa wingi.

"Tunashukuru kwa hatua kubwa ambazo Serikali yetu chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imekuwa ikizichukua kukabiliana na hali iliyopo ambayo hata hivyo nakiri kusema kuwa Tanzania tuna hali nzuri ya mafuta ikilinganishwa na mataifa mengine ya jirani" ,amesema Dkt. Sajad Habib Rai.

Amesema ukweli ni kuwa kupanda kwa bei ya mafuta ni hali inayoikabili Dunia nzima hatua inayosabababisha kuongezeka kwa gharama za maisha huku akisisitiza kwa upande wa Tanzania upo nafuu wa kiasi fulani kutokana na ruzuku ambayo Serikali imeiweka hasa kwa upande wa mafuta ya Dizeli.

"Naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan  kwa jitihada mbalimbali ambazo ameendelea kuzichukua kukabiliana na hali ya kupanda kwa bei ya mafuta Duniani, hii ni kwa namna gani inaonesha uungwana alionao kwa wananchi wake" amesema Dkt. Sajad.

Amesisitiza wao kama wadau katika sekta hiyo ya mafuta, wataendelea kuiunga mkono Serikali na kushirikiana nayo katika hatua mbalimbali kuhakikisha Taifa linapiga hatua kimaendeleo.

Aidha kwa upande wao baadhi ya madereva wa daladala waliozungumza kuhusu suala la mafuta akiwemo Shabaan Haruni wameniomba Serikali kuendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto ya bei ya mafuta nchini.

Amesema kama watoa huduma za Usafiri, wanapata wakati mgumu wa kukamilisha hesabu zao kwa kuwa kiasi kikubwa cha fedha wanayoipata kwa siku hutumika kwenye mafuta tofauti na ilivyokuwa hapo zamani.

Naye Mussa Abdalla ambaye ni Dereva wa bodaboda amesema ingawa kwa sasa wanapitia katika kipindi kigumu, anaamini kuwa hali hiyo itakwisha na maisha yatarudi tena kuwa kawaida.


Post a Comment

0 Comments