KAMPUNI YA MWIBA NA CHAIR THE LOVE WAREJESHA FURAHA SERENGETI WAKITOA VITI MWENDO


  Na Mwandishi wetu,Serengeti. 

 Kampuni kitalii ya Mwiba Holdings Ltd kwa kushirikiana na Shirika la Marekani la Chair the Love wametoa msaada wa viti mwendo 75 kwa wenye changamoto za kutembea.      

Msaada huo ni mfululizo wa misaada ya kijamii ambayo Chair the Love wamekuwa wakishirikiana na taasisi za uhifadhi nchini Tanzania kusaidia jamii ambazo zinaendeleza uhifadhi wa mazingira na Wanyama pori.

Kabla ya kutolewa viti hivi Kwa wenye uhitaji Serengeti shirika hilo pia lilitoa viti kwa kushirikiana na Taasisi ya Chem Chem ambayo imewekeza shughuli za Utalii wa picha na hoteli katika eneo la hifadhi ya jamii ya Wanyamapori ya Burunge (Burunge WMA) wilaya ya Babati mkoa wa Manyara .

Shirika hilo pia  kwa kushirikiana na Kampuni ya Mwiba holdings ltd iliyowekeza shughuli za Utalii wa picha ma hoteli wilaya ya Meatu ilitoa viti eneo la hifadhi la  Makao wilayani Meatu mkoani Simiyu.

Wakazi 75 waishio vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Ikoma( Ikona WMA) na Ikorongo kutoka katika Wilaya za Serengeti na Bunda wenye ulemavu wa viungo mbalimbali nao sasa walifikiwa juzi na  kurejeshewa tabasamu 

Akizungumza wakati wa kugawa baiskeli.hizo, Sylvester Bwasama Meneja Miradi wa Friedkin Conservation Fund,inayomiliki kampuni ya Mwiba Holdings ltd  alisema msaada huo umetokana na safari yenye matokeo chanya kutoka kwa watalii kutoka Nchini Marekani na umelenga kusaidia jamii ya waishio pembezoni.

“Hii ni awamu ya tatu tulianzia Babati kisha Meatu na leo tupo Serengeti, tunatarajia viti vilivyotolewa kwa ajili ya watoto,wanawake na wanaume tunaamini vitawasaidia kwa namna moja,zoezi hili ni litaendelea kwa ambao hawajafikiwa siku ya leo”alisema.

Bwasama alisema, msaada huo umetokana na faida za uhifadhi wa mazingira na wanyamapori kwa jamii ambazo zipo karibu na hifadhi za Taifa.

 Katibu wa IKONA WMA,Yusuph Manyanda  alishukuru taasisi ya Friedkin kupitia Mwiba kwa kurejesha furaha kwa wananchi ambao walikuwa wamekata tamaa .

Alisema msaada huo unathibitisha matunda ya uhifadhi hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kutunza mazingira na wanyamapori.

 “Kama taasisi ya uhifadhi tumetumia fursa ya wageni wanaotembelea maeneo yetu kuisaidia jamii, sasa uhifadhi unamgusa mwananchi moja kwa moja ni imani yangu vitimwendo hivi vitawawezesha kufika maeneo mbalimbali ya kijamii” alisema


Alisema,kama kusingekuwa na utalii marafiki kutoka Chair the Love wa Marekani na Friedkin   wasingefika na kusaidia jamii,hivyo akasisitiza  jamii ijitahidi kulinda na kuhifadhi maliasili zilizopo kwa kuwa faida zake ni kubwa sana kwa kuwa zinagusa kila kundi.


Akipokea na kukabidhi viti hivyo Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Angelina Marko amesema serikali imendelea kuweka mikakati imara kwa ajili ya kuwasaidia walemavu ikiwemo mikopo yenye riba nafuu sambamba na kuwajengea miundombinu ya elimu.

“Leo tumepata watalii wanaounga jitihada za serikali, niwaombe wawekezaji wengine tuige mfano wa Mwiba  na tuendelee kuwa wahifadhi wazuri” alisema.

Mwakilishi wa Shirika la Chair The Love Glen Mother alisema,wanafanya utalii pamoja na kusaidia jamii yenye mahitaji maalum Duniani kote,”tuko wengi lakini kwa hapa tumeteuliwa watu 15 kuja Tanzania,tunaomba sana wanaowahudumia watu kama hawa wawe na moyo wa upendo,”amesema.

Monica Mugabo Mkazi wa Kijiji cha Nattambiso mmoja wa wanufaika alishukuru taasisi ya Friedkin kwa kiwezesha wao kufikiwa na kupata msaada.

 “Sikutegemea kama nitapata kiti kama hiki, ninawashukuru wadau hawa kitaniwezesha kufika ibadani kwa urahisi na kufanya shughuli za kiuchumi”amesema.

Kwa mwaka wa nne sasa shirika la Chair the Love limekuwa likitoa viti mwendo kwa kushirikiana na taasisi za uhifadhi hapa nchini.

Post a Comment

0 Comments