WOMEN FUND TANZANIA YAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI 2026


Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2026, Shirika la Women Fund Tanzania limeandaa kongamano maalum la kujadili masuala ya usawa wa kijinsia na mabadiliko ya tabia nchi.

Kongamano hilo lililofanyika Machi 30, 2026 mkoani Tanga limeandaliwa kupitia mradi wa ReSea unaotekelezwa kwa ushirikiano na Mission Inclusion, IUCN Tanzania, huku ukifadhiliwa na Global Affairs Canada.

Kongamano hilo lililenga kuleta pamoja sauti za wadau na wana mabadiliko ili kutafakari na kuhamasisha haki za mazingira ndani ya uchumi wa buluu jumuishi ambapo Kauli mbiu ya kongamano hilo ni “Kuendeleza Uchumi wa Buluu unaozingatia Usawa, Haki na Maendeleo Shirikishi kwa Ustawi wa Mazingira.”

Kongamano hilo lilihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo vikundi vya uchumi wa buluu vinavyonufaika na mradi wa ReSea kutoka maeneo ya Pemba na Tanga, viongozi wa serikali kutoka wizara husika pamoja na wawakilishi wa mashirika na watetezi wa haki za wanawake, wasichana na watoto.

Miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa ni pamoja na maonyesho ya bidhaa za wajasiriamali wa vikundi vya uchumi wa buluu waliowezeshwa na mradi huo, uwasilishaji wa uchambuzi wa kijinsia katika sera za uchumi wa buluu, pamoja na majadiliano ya kina kuhusu sauti za mabadiliko, changamoto za kisera na uzoefu wa kijamii katika utekelezaji wa shughuli za uchumi huo.



Post a Comment

0 Comments