WANAFUNZI WASISITIZWA MAADILI, UZALENDO KUELEKEA MASHINDANO YA UMISETA

Na Shaban Njia, KAHAMA.

WANAFUNZI wa shule za sekondari katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wameaswa kuzingatia maadili, kuonyesha uzalendo na kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha wakati wote wa mashindano ya michezo ya UMISETA ili kudumisha nidhamu na kulinda amani.

Aidha wito huo umetolewa kwa wanafunzi kutoka shule za sekondari za Isagehe, Kagongwa, Bugisha, Iyenze, Mpera pamoja na Good Hope.

Akizungumza leo katika Kata ya Isagehe wakati wa zoezi la kuunda timu ya wilaya itakayoshiriki mashindano ya UMISETA, Ofisa Utamaduni wa Manispaa ya Kahama Martha Fidelis, amesema ni muhimu kwa wanafunzi kuzingatia maadili na kujiepusha na vitendo viovu vinavyoweza kuvuruga amani wakati wa mashindano.

Amesema mashindano hayo siyo tu jukwaa la kuonyesha vipaji vya michezo bali pia ni nafasi ya wanafunzi kuonyesha nidhamu, mshikamano na uzalendo kwa taifa lao.

Aidha amewataka wanafunzi kuenzi na kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha wakati wote wa michezo na kusisitiza kuwa lugha hiyo ni utambulisho wa taifa na chombo muhimu cha mawasiliano kinachopaswa kuheshimiwa na kutumika ipasavyo.

Naye Ofisa Michezo wa Manispaa hiyo Lupola Mkomwa, amewahimiza wanafunzi kujituma katika michezo, kusikiliza maelekezo wanayopewa na walimu na makocha wao na kutumia fursa hiyo kuonyesha vipaji vyao kwa nidhamu na uadilifu.

Pia amewataka kuendelea kufanya mazoezi kwa bidii ili kupata timu imara itakayoweza kushindana vyema na kuleta ushindi kwa wilaya hiyo.

Mkomwa amesema wanapaswa kuzingatia usafi, nidhamu na ushirikiano muda wote watakapokuwa kambini ili kuhakikisha maandalizi ya mashindano yanaenda vizuri na kwa mafanikio.


Post a Comment

0 Comments