BENKI YA TIB NA EADB ZATEMBELEA NA KUSHUHUDIA MAFANIKIO YA PIPES INDUSTRIES JIJINI DAR ES SALAAM

      

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Benki ya Maendeleo (TIB) leo ilimkaribisha rasmi Meneja Mkazi (Country Manager – Kenya) mpya wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Bi. Angela Muga na ujumbe wake kwa ziara maalumu yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Taasisi za Fedha za Maendeleo (DFIs) katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika ziara hiyo iliyoambatana na ujumbe kutoka benki ya EADB, imeonyesha dhamira ya pamoja ya kuharakisha ukuaji endelevu wa uchumi, kubadilishana uzoefu, ujenzi wa viwanda na ujumuishaji wa kikanda katika eneo la Afrika Mashariki.

Ujumbe wa Bi. Muga ukiongozwa na mwenyeji wake Bw. Stephen Wambura ambaye ni Meneja Mkazi EADB Tanzania, pia ulipata nafasi ya kufanya ziara katika kiwanda cha kuzalisha mabomba ya plastiki cha Pipes Industries kilichopo eneo la viwanda la Vingunguti jijini Dar es Salaam ambapo kiwanda hicho ni mnufaika muhimu wa ufadhili huo wa pamoja.
Kiwanda cha Pipes Industries kilipokea mkopo wa takribani Shilingi za kitanzania Bilioni 28.65, ambao umekuwa na mchango mkubwa katika kupanua uwezo wake wa uzalishaji na kuimarisha shughuli zake.

Mtaji huo umeiwezesha kampuni kuongeza uzalishaji wa bidhaa muhimu za plastiki, ikiwemo mabomba yenye umuhimu mkubwa kwa miundombinu ya usambazaji wa maji mijini na vijijini.Kiwanda hicho kimeleta matokeo muhimu ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuzalisha ajira kwa Watanzania, kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi na kuboresha upatikanaji wa vifaa vya miundombinu ya maji vinavyosaidia mitandao ya usambazaji wa maji.

Uwekezaji huu unaendana na mkakati mpana wa Tanzania wa ujenzi wa viwanda kwa kukuza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
Kwa kuunga mkono kiwanda kama cha Pipes Industries, TIB inaendelea kuwa na mchango muhimu katika kuimarisha sekta binafsi na kuongeza ustahimilivu wa uchumi.Akizungumza wakati wa ukaribisho huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo TIB, Bw. Deogratius Kwiyukwa, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za fedha za maendeleo za kikanda katika kuhamasisha mitaji ya muda mrefu kwa ajili ya miradi yenye kuleta mabadiliko.Kwiyukwa alisema, “Ni furaha kubwa kwetu kumkaribisha rasmi ofisini kwetu Bi. Angela Muga, Meneja Mkazi mpya wa Benki ya Maendeleo Afrika Mashariki (EADB Kenya). Ushirikiano wetu huu ni wa muda mrefu zaidi ya miaka 10 ambapo kupitia EADB, TIB imeweza kutoa fedha za miradi zenye jumla ya thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 80 ambazo zimegawanywa kwenye sekta mbalimbali zikiwemo; kilimo, afya, elimu, viwanda, madini na utalii.”Kwiyukwa alisisitiza, “Kupitia ushirikiano huu, zaidi ya shilingi Bilioni 28 zimewekezwa katika mradi wa upanuzi wa Kiwanda cha Mabomba ya plastiki cha Pipes kilichopo Vingunguti Dar es Salaam ambapo matokeo ya uwekezaji hu oni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa za plastiki kama mabomba ya maji, ajira kwa vijana wakike na wakiume na kukuza sekta ya viwanda nchini.”

Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa Benki ya EADB Bi. Angela Muga alisema, “Ushirikiano miongoni mwa Taasisi za Fedha za Maendeleo ni muhimu katika kufungua fursa za mitaji mikubwa kwa ajili ya mabadiliko ya kikanda. Kwa kuoanisha rasilimali zetu tunaweza kuharakisha ukuaji wa viwanda, kuimarisha ujumuishaji wa kikanda na kuleta matokeo endelevu kwa Afrika Mashariki.”

Aidha aliongeza, “Mwenendo huu unaokua wa ushirikiano kati ya taasisi za fedha za maendeleo unaonekana kupitia juhudi za pamoja kati ya taasisi kama Benki ya Maendeleo ya TIB na EADB, ambazo zinaendelea kuhamasisha mitaji ya muda mrefu kwa ajili ya miradi yenye kuleta mabadiliko nchini Tanzania na katika ukanda mpana zaidi.”Ushirikiano kati ya TIB na EADB unaonesha kukua kwa nafasi ya taasisi za kifedha za kikanda.

Kwa kutoa mitaji ya muda mrefu yenye uvumilivu, taasisi hizi zinajenga minyororo muhimu ya kuongeza thamani ambayo inaendelea kuleta matokeo chanya hata baada ya kipindi cha ufadhili kumalizika.

Kuhusu Benki ya Maendeleo TIB, Benki ya Maendeleo TIB ni taasisi ya Serikali na ni ya kisera, imeundwa mahususi kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya uwekezaji wa ndani ya nchi hususani katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya Serikali na miradi ya sekta binafsi.

Benki inalenga sekta za kipaumbele ikiwemo miundombinu, kilimo, viwanda na uzalishaji, madini, utalii, uchumi wa buluu pamoja na biashara ndogo na za kati (SMEs).
Aidha, Benki ina jukumu muhimu katika kusimamia mifuko ya maendeleo na kusaidia maandalizi ya miradi ili kuibua uwekezaji unaochochea ukuaji endelevu wa uchumi wa Tanzania.

Kuhusu EADB, Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) ilianzishwa mwaka 1967 chini ya mkataba wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo. Dhamira yake ilikuwa kutoa msaada wa kifedha na huduma zinazohusiana kwa makampuni katika nchi wanachama ambayo, kupitia shughuli zao, yalitarajiwa kutoa mchango chanya katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika ukanda huo. Benki ilianzishwa upya chini ya Hati mpya mwaka 1980.

Chini ya Hati hiyo, jukumu na dhamira ya Benki vilipitiwa upya na wigo wa shughuli zake kupanuliwa kujumuisha huduma mbalimbali za kifedha katika nchi wanachama, ikiwa na lengo kuu la kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na ujumuishaji wa kikanda. Kwa sasa, EADB inamilikiwa na nchi nne wanachama ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda pamoja na taasisi nyingine za maendeleo na kifedha za kibiashara. Ikiwa ni chombo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kupitia ushirikiano wake na taasisi za EAC, imepata jukwaa la kuchochea ujumuishaji wa kikanda kupitia utoaji wa fedha za maendeleo.

Post a Comment

0 Comments