Mwenyekiti wa Kikundi cha Better Together Mussa Ngangala akikata keki wakati wa uzinduzi rasmi wa Kikundi cha Better Together katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ameongoza uzinduzi rasmi wa Kikundi cha Better Together katika hafla iliyogubikwa na shamrashamra, nderemo na vifijo vya wanachama waliojaa matumaini na mshikamano huku akikipongeza kikundi hicho kwa maono yake ya kuimarisha umoja, ustawi wa kijamii na kukuza maendeleo ya kiuchumi miongoni mwa wanachama wake.
Uzinduzi huo ulifanyika tarehe Februari 14, 2026 ulitanguliwa na shughuli za kijamii na kiafya zikiwemo mbio za amani (jogging) zilizoanzia Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kuhitimishwa katika Uwanja wa CCM Kambarage, sambamba na mazoezi ya viungo (aerobic na cardio).
Wanachama pia walitembelea Kituo cha Afya Kambarage na kutoa matendo ya huruma kwa wagonjwa na wahitaji, kabla ya kuhitimisha siku hiyo kwa sherehe rasmi ya uzinduzi jioni katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mtatiro alisema kuwa vikundi vya kijamii kama Better Together vina mchango mkubwa katika kuimarisha mtaji wa kijamii, kusaidiana wakati wa changamoto na kujenga utamaduni wa uwajibikaji.
“Nawapongeza sana waanzilishi na wanachama wa Better Together kwa maono yenu. Kuanzisha na kuendesha kikundi chenye wanachama zaidi ya 400 ndani ya muda mfupi ni ishara ya uongozi makini na imani ya watu. Serikali inaamini katika nguvu ya umoja wa wananchi. Endeleeni kushikamana, kudumisha nidhamu ya fedha na uwazi ili kikundi chenu kiwe mfano bora wa kuigwa,” alisema Mtatiro.
Aliongeza kuwa, vikundi vinapojengwa katika misingi ya uaminifu, husaidia kupunguza mzigo wa kijamii kwa familia na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ngazi ya chini.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Better Together, Mussa Jonas Ngangala, alisema uzinduzi huo ni hatua muhimu katika safari ya kuimarisha taasisi yao na kuongeza wigo wa huduma kwa wanachama.
“Tulianza kama wazo la kuinuana katika changamoto za maisha, lakini leo tumekuwa familia kubwa yenye wanachama zaidi ya 400. Dhamira yetu ni kujenga mfumo imara wa kusaidiana kijamii na kiuchumi, kuhakikisha kila mwanachama anahisi kuthaminiwa na kulindwa katika nyakati za shida na furaha,” alisema Ngangala.
Alibainisha kuwa kikundi kitaendelea kuandaa programu za kijamii, kuhamasisha utunzaji wa afya, pamoja na kuendeleza utamaduni wa kuchangia na kusaidiana kwa uwazi na uwajibikaji.
Better Together ni muunganiko wa wanachama zaidi ya 400, wengi wao wakiishi Mkoa wa Shinyanga huku wengine wakitoka nje ya mkoa huo. Kikundi hicho kilianzishwa mwezi Oktoba 2025 kwa lengo la kusaidiana katika nyakati za shida na raha, pamoja na kufanya matendo ya huruma katika jamii.
Katika hafla hiyo, wanachama pia walifanya harambee ya kuchangia mfuko wa kikundi ili kuimarisha uwezo wake wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi zaidi mwaka 2026.
Uzinduzi wa Better Together umeweka msingi wa kuendelea kujenga mshikamano, kuimarisha mtandao wa kijamii na kukuza ustawi wa wanachama wake, huku ukiwa mfano wa namna vikundi vya kijamii vinavyoweza kuwa chachu ya maendeleo katika jamii.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Kikundi cha Better Together katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga

Mwenyekiti wa Kikundi cha Better Together Mussa Ngangala akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Kikundi cha Better Together katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga
Mwenyekiti wa Kikundi cha Better Together Mussa Ngangala (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro wakati wa uzinduzi rasmi wa Kikundi cha Better Together katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga








































0 Comments