KOCHA MPYA SIMBA...WANNE WAPENYA YUPO WA PITSO MOSIMANE

MABOSI wa Simba wanaendelea kukuna vichwa kuhusu kumpata kocha mkuu mpya wa timu yao ili kuchukua nafsi iliyoachwa wazi na Mfaransa, Didier Gomes kutokana na ngoma kuwa nzito kwa majina na wasifu (CV) ya makocha waliotuma maombi kwao.

Habari kutoka ndani ya Simba zilizothibitishwa na baadhi ya vigogo wa klabu hiyo ni kwamba hadi juzi Jumamoi, jopo maalum linalosimamia mchakato huo wa kutafuta kocha, lilifanya mchujo wa awali wa makocha 100 walioomba kazi na kupitisha wanne, huku zoezi likitarajiwa kuendelea leo.

Inaelezwa jopo hilo litarudi tena kwenye majina hayo 96 yaliyobaki kutafuta majina mengine sita ili kupata 10 bora ya makocha wenye sifa wanazozitaka ili mwishowe waje kushindanisha kupata tano bora, kisha tatu bora na mwisho atakayemrithi Gomes aliyeinoa timu hiyo kwa muda wa miezi tisa tu.

Miongoni mwa makocha wanne wa awali waliopenya mchujo huo ni Rhulani Mokwena wa Afrika Kusini anayepewa nafasi kubwa kutokana na kupendekezwa na kocha mkubwa Afrika, Pitso Mosimane aliyepo Al Ahly ya Misri ambaye alifanya kazi na kocha huyo bingwa wa Afrika wakati wakiwa pamoja Mamelodi Sundowns).

Baada ya Mokwena kuna kocha wa Afrika mwingine mmoja (jina bado halijafahamika) sambamba na Mjerumani, Josef Zinnbauer na Muargentina Miguel Angel Gamondi ambaye mwaka jana aliifundisha Wydad Casablanca ya Morocco anayocheza nyota wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva.

Mmoja wa wajumbe katika jopo hilo la kusaka kocha mpya, aliliambia Mwanaspoti kwa sharti ya kutotajwa jina lake gazetini kwamba mchujo mwingine utafanyika leo Jumatatu na kupata makocha sita ambao kati ya hao watano watakuwa Waafrika na mmoja ni mzungu.

“Baada ya hapo tutafanya mchujo mwingine na kupata watatu bora na tutafanya kikao nao cha (video conference) na kila mmoja kujibu kwa usahihi maswali ya kiufundi tutakayomuuliza na kueleza falsafa zake zinaendana na mahitaji yetu,” alisema mjumbe huyo na kuongeza;

“Kati ya hao watatu yule ambaye atakuwa katika malengo yetu pamoja na kuuliza watu mbalimbali watakaomuelezea kiufundi huko alipotoka na maeneo mbalimbali ndio tutamchukua na malengo yetu makubwa awe Mwafrika na si lingine.”

Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alisema katika orodha ya makocha walioomba kazi wanahitaji Mwafrika zaidi na si Mzungu kama kama aliyetoka.

“Hakuna Waafrika wengi walioomba kazi hii pengine kwa kuogopa ukubwa wa Simba na mafanikio tuliyoyapata, lakini hata kama akikosekana katika orodha tuliyonayo tayari tumeanza kuwafuatilia makocha wengine wa Afrika,” alisema Barbara na kuongezea;

“Tumewasiliana na makocha wakubwa wametushauri aina ya kocha ambaye tunamuhitaji ndio maana tumepata uamuzi wa kuwa na Muafrika kama huyo Mokwena ambaye kweli ametuma maombi.

“Naona tuna sababu nyingi katika uongozi wetu ambazo zimetufanya kuwa na uamuzi wa awamu hii kutaka kocha wa Afrika mwenye kiu na njaa ya mafanikio hata kama akiwa hafahamiki na wengi na ukubwa wake atakuja kuupata kwetu.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema wanahitaji kocha mwenye mafanikio katika kufundisha soka la Afrika ikiwemo kuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Tunataka kocha mwenye ufundi mwingi, kucheza soka la chini, atakayeifanya Simba iwe na uwezo zaidi, kutupa mafanikio ndani na nje katika mashindano yote na kuleta ushindani,” alisema Try Again.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.