HUKO YANGA.. MUKOKO, MAKAMBO WAWEKWA MTU KATI

YANGA iko kambini wakipiga tizi la asubuhi na jioni wakijindaa na mchezo wa Ligi dhidi ya Azam FC lakini kocha wao Nesreddine Nabi ameshtukia jambo na anachotaka ni kila mchezaji awe na kitu cha kuinufaisha timu yake na haraka akafanya vikao viwili na wachezaji wake wawili mastaa.

Kocha Nabi ameliambia Mwanaspoti kwamba hataki kuona ubora wa wachezaji wake unapishana na kwamba anataka kumpa kila mchezaji nafasi ya kucheza na kufanya kitu katika timu hiyo wafikie malengo ya kuchukua mataji.

Nabi alisema katika akili yake hiyo anajua kwamba mshambuliaji wake Heritier Makambo anataka kucheza sana lakini kitu kimoja ambacho amemwambia alivyofanya naye kikaoni kwamba katika muda anaocheza basi afunge tu.

“Huwezi kuwa na mafanikio kwa kikosi cha wachezaji 11 pekee kila mchezaji kwangu ana umuhimu wake, nimewaambia hata kama hautacheza mechi nitatafuta mechi ya kirafiki ili kila mtu awe sawa, tunahitaji kuwa na watu wanaoshindana kwa usawa katika ubora na sio kupishana,” alisema Nabi.

“Nitampa kila mchezaji nafasi kama nitaona anaonyesha kitu cha kusaidia timu, nimefanya kikao na Makambo nimemwambia nitampa muda wa kucheza lakini nataka afunge tu apambane katika muda ambao anacheza afunge hicho ndio kitu mimi nataka na timu inataka hata mashabiki wakiona anafunga watafurahia,” alisema Nabi.

Aliongeza kuwa mbali na Makambo pia amumuweka pia chini katika kikao tofauti kiungo wake na nahodha msaidizi Mukoko Tonombe kwamba apambane kushindana na viungo wenzake Khalid Aucho na Yannick Bangala na kama akifanya hivyo atapata muda wa kucheza.

“Mukoko ni mchezaji wangu bora naye nimekaa naye katika kikao cha mimi na yeye nimemwambia anatakiwa kupandisha ubora wake kushinda na wenzake, namuamini Mukoko anaweza kupambana timu inamuhitaji hata mimi namuhitaji hapa na anaweza.

“Akiendelea kupanda kuna wakati nitampa nafasi zipo njia nyingi hapa za kutoa nafasi, jambo zuri tuna wachezaji ambao wanaweza hata kucheza kama mabeki ambao sasa tunawatumia katika kiungo tunaweza kubadilisha kitu kama tunaona kuna ulazima wa kufanya hivyo,” alisema.

Kocha Abeid Mziba ‘Tekelo’ ambaye pia ni mshambuliaji wa zamani wa Yanga alisema Makambo sasa anatakiwa kuamka na kuthibitisha imani yake kwa mashabiki na kwamba kama atashindwa kuonyesha kitu Nabi anaweza kuacha kumpa nafasi.

Kocha Edna Lema alisema: “Kocha hawezi kumpanga mchezaji kwa historia yake ya nyuma ataangalia kile anachokionyesha kwa wakati husika.”

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.