POLISI WAWILI WAFARIKI AJALI YA GARI, 9 WAJERUHIWA MBEYA
Askari wa jeshi la polisi wawili wamefariki dunia huku wengine 9 wakijeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea jana jioni katika eneo la Iwambi, Kata ya Iwambi tarafa ya Iyunga jijini Mbeya
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Naibu Kamishina wa Polisi, Mohammed Mpinga amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kudai kuwa jumla ya askari wawili wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa na kusema chanzo cha ajali hiyo ilikuwa ni mwendokasi wa dereva wa gari la polisi alipokuwa akitaka kuyapita magari mengine pamoja na utelezi.
"Mnamo tarehe 18.01.2018 majira ya saa 16:45 jioni huko eneo la Iwambi, Kata ya Iwambi, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya katika barabara kuu ya Mbeya kwenda Tunduma, gari yenye namba za usajili PT 2079 Toyota Land Rover mali ya Jeshi la Polisi Kikosi cha FFU - Mbeya ikiendeshwa na askari namba G. 3452 PC ADAM Mkazi wa Iganzo ikitokea Mbeya Mjini kuelekea Mbalizi iliacha njia na kupinduka kisha kusababisha vifo kwa askari wawili ambao ni 1. H. 4335 PC MATHEW JAILOS MPOGOLE na 2. H. 1215 PC PROSPER JORDAN CHALAMILA "
Aidha katika ajali hiyo, askari 09 walijeruhiwa ambapo kati yao majeruhi wawili wamelazwa Hospitali ya Rufaa Mbeya na majeruhi saba wametibiwa na kuruhusiwa kurudi majumbani kwao Waliolazwa ni 1. H. 6952 PC KELVIN MARTIN Mkazi wa forest ameumia kichwani na 2. G. 3452 PC ADAM Mkazi wa Iganzo, Dereva.
Mbali na hilo majeruhi wengine walitibiwa na kuruhusiwa.
"Chanzo cha ajali ni mwendokasi akijaribu kuyapita magari mengine pamoja na utelezi katika barabara. Upelelezi unaendelea. Miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya na majeruhi wamelazwa Hospitalini hapo. Taratibu za kusafirisha miili ya marehemu kwenda nyumbani kwao Iringa zinafanyika" alisema Mpinga.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: