AKAMATWA AKISAFIRISHA DOLA 123,000 UWANJA WA NDEGE DAR
Mwezi mmoja baada ya kumnasa Mganda akiwa anasafirisha kwa ndege Dola za Marekani milioni moja, Jeshi la Polisi limedai kunasa mfanyabiashara wa vipuri vya magari akiwa na Dola za Marekani 123,000 (Sh. milioni 274.4) dakika chache kabla hajaingia kwenye ndege iliyokuwa inakwenda Dubai.
Kamanda wa Viwanja vya Ndege, Matanga Mbushi, jana alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi saa 9:30 alasiri kwenye eneo la kuondokea 'Terminal II' la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Akieleza zaidi kuhusu tukio hilo, Mbushi alisema polisi kwa kushirikiana na maofisa wa usalama na Mamlaka ya Mapato (TRA) walimkamata abiria huyo, aitwaye Boniface Mbilinyi (32) mwenye hati ya kusafiria AB 757247.
Alisema kuwa mfanyabiashara huyo ambaye ni mkazi wa Tabata Segerea jijini alikuwa anasafiri kwa ndege ya Shirika la Emirates kuelekea Dubai kwa shughuli za kibiashara.
“Baada ya kupita kwenye mashine, alionekana ana fedha nyingi, akaenda kutoa taarifa ya kiasi cha Dola 40,000 badala ya fedha zote na hivyo kiasi cha Dola 83,000 hakukitolea taarifa,” Mbushi alisema.
Aliongeza: "Tunaendelea na mahojiano na iwapo yatakamilika leo (jana), faili litapelekwa kwa mwanasheria kwa ajili ya kufikishwa mahakamani. Kosa lake ni kushindwa kutoa taarifa ya fedha anazosafiri nazo.”
Alipoulizwa kama wameshabaini sababu za mfanyabiashara huyo kushindwa kutolea maelezo fedha hizo, Mushi alisema: "Ni kutokujua sheria. Sheria bado inawasumbua watu, inahitajika elimu watu waelewe kuwa unapokuwa unasafiri kwenda nje ya nchi na fedha nyingi, lazima utoe maelezo ya fedha husika kwa TRA."
Kamanda Mushi alibainisha kuwa mfanyabiashara huyo ni muuzaji wa vipuri vya magari, hivyo alikuwa anakwenda Dubai kununua vifaa hivyo.
Alisema kiasi hicho cha fedha kimehifadhiwa kwenye akaunti ya Dola ya FIU yenye namba 20110028135.
Tukio hilo ni la pili kwa uwanja huo ndani ya kipindi cha takribani mwezi mmoja baada ya Desemba 11 Mganda Winfrida Vusinge kukamatwa na Dola za Marekani milioni moja (Sh. bilioni 2.23) alizokuwa anazileta Tanzania kwa lengo la kuziweka kwenye Benki ya Stanbic.
Kwa mujibu wa Kamanda Mushi, raia huyo wa Uganda tayari alishafikishwa mahakamani kwa kukiuka sheria za nchi.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: